Na Farida Mangube, Morogoro
Katika kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Japan, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) limezindua Kigoda cha JICA katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Kigoda hicho kitakuwa jukwaa la wataalamu kubadilishana ujuzi na kufanya tafiti juu ya mbinu bora za kilimo cha umwagiliaji.
Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia Elimu Msingi, Dkt. Wilson Mahela, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, ambapo akizungumza katika uzinduzi huo Dkt. Mahela amesema kuwa hatua hiyo itasaidia wataalamu kupata mbinu za kisasa, hasa kutokana na mafanikio ya Japan katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji.
“Kilimo cha umwagiliaji kinaongeza uhakika wa chakula na lishe kwa nchi, kwani wakulima watakuwa na teknolojia zinazowawezesha kuzalisha kwa tija kwenye eneo dogo,” amesema Dkt. Mahela.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu - SUA (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu), Prof. Maulid Mwatawala, amesema kuwa kigoda hicho kitaleta mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini.Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mke. Mikami Yoichi, amesema kuwa kigoda hicho kitaimarisha uelewa wa uzoefu wa maendeleo ya Japan na mchango wake kwa Tanzania kupitia mihadhara, semina na tafiti mbalimbali.
Mwakilishi Mkazi wa JICA, Asano Seizaburo, ameongeza kuwa kigoda hicho ni fursa muhimu ya kubadilishana utaalamu na kusaidia kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji nchini Tanzania.
Kongamano hili linafanyika kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa.
0 Comments