Header Ads Widget

FRANKFURT ZOOLOGICAL SOCIETY (FZS) BEGA KWA BEGA NA TANAPA KATIKA UHIFADHI



Na. Edmund Salaho – Arusha


Shirika la Kimataifa linalojihusisha na Uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS) limeendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika Uhifadhi wa Maliasili katika Hifadhi za Taifa Nchini ambapo leo Februari 10, 2025 wamekabidhi gari moja lori aina ya ISUZU kwa TANAPA chini ya mradi wa Dharura wa Uhifadhi na Utalii Tanzania (Emmergency and Recovery Support for Biodiversity (ERB).


Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika ofisi za TANAPA Makao Makuu jijini, Arusha, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa aliipongeza FZS kwa namna ambavyo imekuwa ikisaidia juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia TANAPA katika Uhifadhi na Utalii.


“Serikali ya Tanzania kupitia Shirika lake la TANAPA imekuwa na ushirikiano mzuri na Serikali ya Ujerumani kupitia FZS kwa takribani miaka sitini sasa katika kuhifadhi kuendeleza jamii. TANAPA tunaamini kwamba hatuwezi kuhifadhi bila kuigusa jamii, ni lazima jamii inufaike, Hivyo kupatikana kwa gari hili kutasaidia katika shughuli za Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Serengeti”


“Gari hili litatumika kuchukua vikundi vya kijamii kutoka katika maeneo yao na kuwaleta katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kujifunza shughuli za Uhifadhi na Utalii lakini pia litatumika kusafirisha kikundi kimoja cha kijamii kwenda kikundi kingine kwa lengo la kujifunza zaidi” alisema Kamishna Mwishawa.


Aidha, Kamishna Mwishawa alimtaka Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi, kuhakikisha gari hilo linaelekezwa kwenye matumizi stahiki na kuhakikisha kwamba linatunzwa vizuri ili kuleta tija iliyokusudiwa.


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Frunkfurt Zoological Society (FZS), Dkt. Ezekiel Dembe ameeleza kuwa FZS itaendelea kushirikiana na TANAPA katika kuendeleza juhudi za Uhifadhi na utunzaji wa Mazingira nchini.


“Lengo letu ni kuona TANAPA inakwenda mbele zaidi katika Uhifadhi. Tunaahidi ushirikiano zaidi katika Uhifadhi na Maendeleo ya Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizi zinapaswa kutuzwa vizuri endapo tutaziharibu tufahamu kuwa tumeharibu mazingira, na mazingira yanayo namna yakutuadhibu na hata vizazi vijavyo vitatulaumu kwa kutotunza Mazingira vizuri” alisema Dkt.Dembe 


Andrew Mwakisu ambaye ni Mratibu wa Mradi wa ERB kutoka FZS alibainisha kuwa mradi huo umekuwa na manufaa makubwa katika shughuli za Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, na Nyerere.


“Hifadhi ya Serengeti kwa kweli imebahatika kupata malori manne ikiwemo mawili kwa shughuli za kawaida za Uhifadhi, lori moja kwa ajili ya kubeba wanyama na sasa hili ambalo tunalitoa leo lilikuwa limebakia kati ya yale malori nane likiwa ni kwaajili ya Ujirani Mwema.”


 “Mradi wa ERB umefanya mambo mengi tumeweza kununua magari na vifaa mbalimbali hili ni lori la Nane sasa, malori mengine yalikwenda Selous, Nyerere, na Serengeti. Ikiwa ni mwaka wa mwisho wa mradi huu tumeona ufanisi mkubwa katika maeneo yanayofaidika na mradi huu”.


FZS imekabidhi kwa TANAPA lori aina ya ISUZU linaloweza kubeba watu 30 kwa wakati mmoja likiwa na thamani ya dola za kimarekani 177,966/= linaloenda kutumika na Idara ya Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.










Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI