Header Ads Widget

WAZIRI WA UGANDA AOMBA TANZANIA IONDOE KODI KWA BIDHAA ZA UGANDA

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma 

WAZIRI Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja, alisisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa kibiashara wa kudumu kati ya nchi za Afrika Mashariki, akieleza kwamba hatua ya Tanzania kufuta kodi kwa mchele wa Uganda ilikuwa ni mfano mzuri wa namna ambavyo nchi zinazoshirikiana zinavyoweza kusaidiana ili kukuza biashara na uchumi wa kila upande.

Msisitizo huo ameutoa leo 29  January 2025 ,jijini Dodoma wakati wa zira ya kutembele kiwanda cha Mbolea cha INTRACOM kilichopo katika eneo la Nala. 

 Ameweka wazi kuwa hatua hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili, kwani Uganda itapata soko la uhakika kwa bidhaa zake, na kwa upande mwingine, Tanzania itafaidika na kupanua soko la mchele . 

" Nchi za Afrika zinahitaji kuwa na mikakati madhubuti ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kuhakikisha kuwa zinapata faida kubwa kutokana na rasilimali zinazopatikana katika kanda, " Amesema .

Aidha, Waziri Mkuu Nabbanja amesisitiza kuwa, ili Afrika iweze kufikia maendeleo endelevu, ni muhimu kuwekeza katika sekta ya teknolojia na elimu ili kuendeleza ufanisi wa wakulima na wafanyabiashara.

 Alisema kuwa mabadiliko ya kiuchumi yataweza kufikiwa kwa kuhakikisha kuwa wananchi, hasa wakulima, wanapata elimu na teknolojia za kisasa ambazo zitawasaidia kufanya kilimo bora na cha kisasa, ambacho kitakuwa na tija na kuongeza kipato kwa familia na taifa kwa ujumla. 

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania, Selemani Jafo, amesema kuwa maombi ya Uganda kuhusu kufutiwa kodi kwenye bidhaa baadhi za biashara yanaendelea kushughulikiwa kwa kupitia njia za kisheria na mamlaka za Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Alieleza kuwa vikao vinavyohusiana na suala hili vinaendelea, na kwamba serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kushirikiana na majirani wake kwa ajili ya kufikia malengo ya maendeleo ya kanda.

 Jafo alieleza kuwa ingawa Tanzania inahitaji mapato kutoka kwenye kodi, ni muhimu pia kuhakikisha kuwa biashara inafanyika kwa urahisi na kwa manufaa ya pande zote mbili ili kuongeza biashara na kuimarisha uchumi wa kikanda.

" Tanzania inajitahidi kusimamia masuala ya kodi, inaelewa umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara katika kanda ya Afrika Mashariki, " Mesema Waziri Jafo

Na kuongeza kusema kuwa, "Wakati wa kushughulikia ombi hili, serikali ya Tanzania itaendelea kuzingatia maslahi ya wafanyabiashara na wananchi wake, na itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa biashara inaendelea kuimarika na kuwa na manufaa kwa nchi zote mbili, " Amesema 

Amesema kuwa ziara hiyo ni fursa nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na maendeleo ya kiuchumi kati ya Uganda na Tanzania, na kwamba hatua zilizochukuliwa zitachochea ukuaji wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa INTRACOM , Nduimana Zee, ameelezea furaha yake kuhusu ujio wa Waziri Mkuu wa Uganda, akisema kuwa hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa na kiwanda chao. 

. Zee alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kumalizika hivi karibuni, na kuongeza kuwa uwekezaji huu utaleta tija kubwa kwa sekta ya viwanda na kusaidia kukuza ajira katika jamii.

"Ujio wa viongozi hawa wa kisiasa ni ishara ya kutambua mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya nchi na kanda kwa ujumla, na kwamba ushirikiano wa kibiashara utaongeza uwezo wa viwanda kama vya Intracom kufikia masoko ya kimataifa, " Amesema.

Zee pia amesisitiza umuhimu wa kukuza mazingira ya biashara ya kirafiki, akisema kuwa hii itachochea maendeleo ya kiuchumi na ufanisi wa viwanda, hasa katika nchi za Afrika Mashariki.

Ameweka wazi kuwa utayari wa serikali ya Uganda kusaidia biashara za kiwanda cha Intracom ni hatua muhimu katika kukuza ushirikiano wa kibiashara, na kuleta maendeleo kwa sekta ya viwanda katika kanda ya Afrika Mashariki.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI