Na Deogratius Temba, Same
Halmashauri ya Wilaya ya Same imeahidi kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia uanzishwaji wa Kamati za MTAKUWWA katika vijiji vilivyosalia, huku Serikali pia ikiahidi kuendeleza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ili kuongeza upatikanaji wa haki katika jamii.
Ahadi hiyo ilitolewa wakati wa mkutano wa mrejesho wa mchakato wa uraghibishi uliofanyika katika Kata ya Maore, uliohusisha wananchi wa vijiji vya Maore, Mpirani, Kadando na Mheza, waliowasilisha changamoto na mapendekezo ya maendeleo yaliyobainishwa kupitia mfumo wa U-Tatu wa Uibuaji, Uchambuzi na Utatuzi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Gibson Mhagama, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Charles Anatory, alisema Halmashauri itaendelea kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuhakikisha Kamati za MTAKUWWA zinaanzishwa katika vijiji vyote ambavyo bado hazijaanzishwa ili kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto pamoja na kukuza uwajibikaji katika jamii.
"Tunaendelea kushirikiana na TGNP kwa sababu matokeo yake yanaonekana. Tutahakikisha Kamati za MTAKUWWA zinaanzishwa katika vijiji vilivyosalia ili wananchi wapate mifumo madhubuti ya kushughulikia ukatili wa kijinsia na changamoto nyingine za kijamii," alisema Anatory.
Aliishukuru TGNP kwa kuendelea kujenga uwezo wa vikundi vya wananchi kupitia Mradi wa Wanawake wa Vijijini Kuongoza Mabadiliko Chanya katika Jamii (WRCC), akibainisha kuwa hatua hiyo imeongeza ushiriki wa wananchi katika kupanga na kusimamia maendeleo yao.
Aidha, alisema kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) katika Kata ya Vumari kumekuwa mfano wa mafanikio kwa kuwa kimeongeza ufuatiliaji wa kesi za ukatili wa kijinsia na kuhakikisha waathirika wanapata haki zao hadi mwisho wa mchakato.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali wa Wilaya ya Same, Upendo Kivuyo, alisema Serikali itaendelea kuimarisha programu ya msaada wa kisheria kwa jamii, hususan katika Kata ya Maore, ili wananchi waweze kupata huduma za ushauri na uwakilishi wa kisheria kwa wakati.
Alisema programu hiyo itaweka mkazo katika kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia, migogoro ya mirathi, migogoro ya ardhi pamoja na migogoro ya mali, ambayo imeendelea kuwa chanzo cha migawanyiko na ukiukwaji wa haki za wanawake na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
"Lengo letu ni kuhakikisha haki inawafikia wananchi bila kujali uwezo wao wa kifedha. Tutaendelea kutoa elimu ya sheria na msaada wa kisheria ili wananchi wajue haki zao na namna ya kuzidai kwa mujibu wa sheria," alisema Kivuyo.
Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na maarifa (KC) Kata ya Maore, Mwanaisha Mramba, alisema mafunzo na uwezeshaji unaotolewa kupitia TGNP umeongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na haki za wanawake, hali iliyochangia kuongezeka kwa utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa kesi.
"Tunaona mabadiliko makubwa katika jamii. wananchi wameanza kuvunja ukimya na kuripoti matukio ya ukatili kwa wakati, huku viongozi wa vijiji na taasisi mbalimbali wakishirikiana kuhakikisha wahanga wanapata msaada na haki zao. Tunahitaji juhudi hizi ziendelee na Kamati za MTAKUWWA ziimarishwe katika kila kijiji," alisema Mramba.
Katika risala yao, Waraghibishi wa Mradi wa Wanawake wa Vijijini Kuongoza Mabadiliko Chanya katika Jamii (WRCC) waliibua changamoto mbalimbali zinazoikabili Kata ya Maore, ikiwemo upungufu wa maji safi na maji ya umwagiliaji, ukosefu wa ofisi ya kata, miundombinu duni ya barabara, mazingira yasiyo salama ya biashara, ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, ndoa na mimba za utotoni, utoro wa wanafunzi pamoja na changamoto za huduma za afya na elimu.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa ni kuimarishwa kwa Kamati za MTAKUWWA katika vijiji vyote, kuboresha huduma za maji na afya, kujenga soko la kisasa, kutenga bajeti ya upangaji na upimaji wa ardhi, kuboresha miundombinu ya shule na kuanzisha mfumo wa pamoja wa kufuatilia utekelezaji wa maazimio hayo.
Mradi wa WRCC unatekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na PELUM Tanzania katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake wa vijijini kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia kilimo ikolojia.











0 Comments