Na Moses Ng'wat, Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amewataka viongozi na watendaji wa Wilaya ya Songwe kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wawekezaji badala ya kutumia njia za kufunga migodi.
Chongolo alitoa wito huo Januari 27, 2025, alipotembelea Mgodi wa Dhahabu wa Dermexim Limited uliopo eneo la Patamela, wilayani Songwe, ili kujionea shughuli za uchimbaji na kuzungumza na wachimbaji, akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani humo.
Kwa mujibu wa wachimbaji, changamoto zinazowakabili ni pamoja na mivutano ya mara kwa mara baina yao na viongozi na watendaji wa serikali, hali wanayodai kuathiri utendaji kazi wa migodi na uwekezaji katika sekta ya madini.
Kufuatia hali hiyo, Chongolo alisisitiza kuwa ni jukumu la viongozi kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji yanaimarishwa ili wawekezaji waendelee kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji, ikiwemo kulipa kodi.
Hata hivyo, Chongolo ameipongeza Kampuni ya Dermexim Limited kwa kuwa sehemu ya walipa kodi wazuri kupitia sekta ya madini serikalini.
Awali, akisoma taarifa ya kampuni hiyo, Mkuu wa Utumishi wa Mgodi, Ramadhan Ally, alisema kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2012, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 12.5 katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu. Aidha, kampuni hiyo imekuwa mshindi wa kwanza kwa ulipaji wa kodi wilayani Songwe kwa miaka miwili mfululizo (2021/2022 na 2022/2023).
"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa katika mwaka wa fedha wa 2024, Dermexim Limited imelipa zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kama kodi na ada mbalimbali za serikali" alifafanua zaidi Ally.
Ally alisema kuwa, kampuni hiyo imeajiri zaidi ya vijana 150 wa Kitanzania na inatumia teknolojia za kisasa, ikiwemo mitambo ya CIP.
0 Comments