Shemsa Mussa -Matukio daima Media
Kagera.
Waandishi wa habari Mkoani Kagera wamepatiwa elimu juu ya ugonjwa wa MARBURG huku wakitakiwa kuwa kipaumbele katika kujikinga na Maradhi hayo.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa huo Mhe Bi Hajjat Fatma Mwasa ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika semina hiyo amewataka Waandishi wa habari waliopatiwa Mafunzo kuhakikisha wanaandika habari zao kwa weledi na zenye uhakika ili kuondoa taharuki inayoweza kujitokeza katika jamii.
Aidha amesema kuwa Waandishi wa habari ni kundi muhimu katika kufikisha taarifa kwa wananchi katika kukabiliana na Janga hili,kwa maslai mapana ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kujiepusha na misongamano ya watu isiyo ya lazima hasa kwenye misiba na sherehe hali inayoweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa huu.
Nae mwakilishi kutoka Shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF Bi Edna Moturi amesema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania pamoja na idara ya Afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Marburg na magonjwa mengine ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.
Pia kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara ya Afya Bw Ntuli kapolongwe amesema kuwa wanao wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuepuka imani na taarifa potofu juu ya ugonjwa huo.
Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa MARBURG ulitangazwa na Mhe Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 20 Jan 2025 kwa mtu mmoja kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo katika wilayani Biharamuro Mkoani Kagera.
0 Comments