Na MWANDISHI WETU, MATUKIO DAIMA App, DAR
MADAI ya malimbikizo ya mishahara ya waandishi wa habari 10 yanaweza kumtupa jela Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Madai hayo ambayo yametua mbele ya Jaji, Dk Modesta Opiyo, waandishi wanaomba mkurugenzi huyo akamatwe aende gerezani.
Wadai wamewasilisha maombi hayo na yamepangwa kusikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Dudley ni Mtoto wa Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, wadai wamefikia hatua hiyo baada ya kushindwa kulipa malimbikizo hayo
Wadai Maregesi Paul na wenzake 9 waliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kumkamata Dudley na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya mishahara yao baada ya kushinda tuzo.
Januari 14 mwaka huu Dudley alionywa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati shauri hilo la madai lilipokuwa likitajwa na kuamuliwa kufika mahakamani na kulipa kabla ya Januari 31,2025.
Wakili Samadani Mngumi aliyemwakilisha Dudley, alidai alikuwa hajazungumza na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru.
Awali Mahakama ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.
Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala, Bonasia Mollel.
0 Comments