Balozi mdogo wa Burundi katika ubalozi mdogo wa Burundi mkoani Kigoma Kekenwa Geremiah
Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
UBALOZI mdogo wa nchi ya Burundi nchini Tanzania umewataka watanzania wanaowatumia raia wa Burundi kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo kilimo kufuata taratibu za nchi katika kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini kwa raia hao ili kuondoa changamoto za kuvunja sheria zinazojitokeza.
Balozi Mdogo wa Burundi katika ubalozi mdogo wa mkoani Kigoma nchini, Kekenwa Geremiah amesema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma Desemba 16 na kubainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la raia wa Burundi kukamatwa na idara ya uhamiaji kwa makosa ya kuishi na kufanya kazi mkoani Kigoma bila kuwa na vibali.
Kukiukwa huko kwa sheria za uhamiaji kunafuatia kubadilishwa kwa taratibu za kuingia na kuishi nchini kwa raia wa Burundi kwa kufuata taratibu za vibali vya ujirani mwema ambapo kwa sasa raia wa Burundi wanatakiwa kuwa na kibali hicho ambacho kitamruhusu kuishi mkoani Kigoma kwa siku 14 badala ya miezi sita iliyokuwepo awali ambapo kwa sasa wanatakiwa pia kutokwenda Zaidi ya kilometa 10 kutoka mpakani.
Balozi Geremiah alisema kuwa watanzania wengi wanawaingiza nchini raia wa Burundi na kuwatumia kwa shughuli zao hivyo muda wa siku 14 unapoishi wanendelea kuishi nao lakini pia kukiwa hakuna mikataba ya kazi baina ya pande hizo mbili jambo ambalo pia limechangia raia hao wa Burundi kudhulumiwa haki zao kwa kazi za vibarua wanazofanya.
Pamoja na hilo Balozi huyo Mdogo wa Burundi nchini alitoa wito kwa raia wa Burundi wanaotaka kuingia mkoani Kigoma nchini Tanzania na kufanya kazi za vibarua kufuata taratibu ambazo ubalozi umetoa maelekezo ili kuzuia changamoto ya kukamatwa kwa makosa ya kuishi na kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali.
Jengo la ubalozi mdogo wa Burundi mkoani Kigoma nchini Tanzania
0 Comments