Header Ads Widget

MAJONZI; MBEYA VIJIJINI WAMLILIA DIWANI BONIFACE NJOMBE, AKIZIKWA

.

Wananchi na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini wamehudhuria ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Diwani wa kata ya Ulenje Mhandisi Boniface Simon Njombe, aliyefariki Dunia Desemba mosi 2024 na kuzikwa Desemba 05, 2024 kijijini kwake Irambo Mbeya vijijini.

Wakizungumza kwenye ibada ya kusindikiza mwili wa marehemu Boniface Njombe, viongozi na waombolezaji mbalimbali wameeleza sifa nzuri ambazo kiongozi huyo alikuwa nazo ndani na nje ya maisha ya siasa.

Katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya Christopher Uhagile, amewataka waumini na wananchi kwa ujumla kuiga matendo mema ya kiongozi huyo ambaye alikuwa mtumishi katika shirika la umeme Tanzania (TANESCO) katika maisha yake ya utumishi huku mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Mwalupindi akisema pengo la kisiasa huwa linazibika lakini tabia ya mtu huwa haizibiki kulingana na kila mmoja alivyoumbwa na Mungu.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Mhe. Mwalingo Kisemba, amesema Diwani huyo alisimamia miradi mbalimbali katika kata yake ikiwemo upatikanaji huduma bora za afya kwa wananchi, upatikanaji huduma ya maji safi, barabara na miundombinu ya elimu.

Akitoa salamu za Serikali ya Wilaya, kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Gideon Mapunda, amesema ni kilio kwa madiwani wa Halmashauri na watumishi wa Halmashauri ya Mbeya kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo hivyo kuwaasa wananchi hasa wa kata ya Ulenje na familia kuendelea kuwa wavumilivu kwenye kipindi hiki kigumu ambapo pia ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbeya imeshiriki ibada hiyo kupitia maafisa Tarafa za Isangati, Utengule Usongwe na Tembela.

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu msaidizi jimbo kuu katoliki la Mbeya Godfrey Mwasekaga iliyofanyika katika kanisa Katoliki Parokia ya Irambo, amehimiza watu bila kujali nafasi zao kuhakikisha wanaishi maisha mema na ya kutenda haki katika maisha yao yote.


Kwa mujibu wa wasifu, marehemu alizaliwa mwaka 1956 na kufariki 2024 ambapo katika uhai wake amefanya kazi katika maeneo na nafasi mbalimbali nchini Tanzania hasa ndani ya Wizara ya nishati ikiwemo kuwa mkurugenzi wa kwanza wa kampuni ya uendelezaji joto ardhi Tanzania (TGDC).

Pia marehemu Mheshimiwa Boniface Njombe, alikuwa akifanya kazi ya Mungu hasa mziki kanisani na kuongoza kamati ya ujenzi katika kanisa la Parokia ya Irambo pamoja na kuwa mwana-siasa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI