Na Thobias Mwanakatwe
WATUMISHI watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamejeruhiwa kwa kupigwa wakati wakiwa katika doria za udhibiti na ukamataji wa magendo na magari yaliyoingia nchini kinyume nataratibu za forodha na kutolipiwa ushuru.
Watumishi hao walishambuliwa wakiwa na gari lao lenye namba za usajili STL 9923 jana katika eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam wakati wakifuatilia gari yenye namba za usajiri T 229 DHZ aina ya BMW X6.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, imeeleza kuwa watumishi hao walikuwa wakiifuatilia gari hiyo baada ya kubaini kuwa iliingizwa nchini kinyemela bila kulipiwa kodi za serikali kwa mujibu wa sheria.
“Walikuwa wanaifuatilia gari hiyo ili waikamate lakini wakati watumihi hao wa TRA wanatimiza wajibu wao walihusishwa na kitendo cha utekaji kilichopelekea wao na gari kushambuliwa,” imeeleza taarifa hiyo.
“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inawapa pole watumishi wake waliojeruhiwa wakiwa wanatimiza wajibu wao pamoja na wengine wote waliojeruhiwa katika kadhia hii na kuwaombea wapone haraka,”
Aidha, TRA imeuhakikishia umma kuwa itaendelea kutimiza wajibu wake kwamujibu wa sheria.
0 Comments