Header Ads Widget

VITONGOJI 90 NDANI YA MAJIMBO SITA YA MKOA WA SONGWE KUNUFAIKA NA UMEME WA REA.

Na Moses Ng'wat, Songwe.

SERIKALI imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 10.84 kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 90 vya majimbo sita ya Mkoa wa Songwe ambapo jumla ya wananchi  2700 wataunganishwa na huduma hiyo .


Hayo yamebainishwa  Septemba 26, 2024 na Mhandisi Herini Mhina kutoka Wakala wa Nishati vijijini (REA) Makao Makuu, wakati wa hafla fupi ya  kumtambulisha kwa Mkuu wa Mkoa Mkandarasi wa kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka Nchini China atakayetekeleza mradi huo.

Mhina alisema mkataba wa utekelezaji mradi huo wa miaka miwili ulisainiwa Agosti 20,2024 na mkandarasi huyo  kutoka China, ambapo utasimamiwa na REA na TANESCO ili kuhakikisha  unatekelezwa kwa viwango huku kila kitongoji kilichopo kwenye mpango huo kinanufaika kama ilivyokusudiwa.


"Mradi huu utakua na laini ndogo ya kilomita 180 ambapo wateja  watakuwa 2700 hivyo tunaahidi kuwa  tutamsimamia mkandarasi amalize kazi ndani ya mkataba ili wananchi wanufaike na mradi," alisema Mhandisi Mhina.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Songwe Mhandisi, Leonard Mtangi, alisema wamejipanga kuusimamia kw ubora mradi huo ili ukamilike kwa viwango vinavyotakiwa huku wananchi wakitakiwa kupisha maeneo ili wapate mradi.


"Huu utakuwa ni mradi wa sita wa umeme kutekelezwa mkoani hapa ambapo miongoni mwake ni mradi wa REA 3 awamu ya pili umevifikia vitongoji 127 vyote vina umeme na umefikia 90% kukamilika, mradi wa umeme jazilizi, mradi wa vitongojini," alibainisha Mhandisi Mtangi.


Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema  tayari vijiji vyote  307 vilishapatiwa huduma ya umeme na kwamba  vitongoji 749 navyo tayari vimewashwa kati ya vitongoji 1489.

 

"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha hizi kiasi cha shilingi Bilioni 10.84 na  leo tunamtambulisha mkandarasi ambaye atapanua wigo wa kuwafikishia wananchi kwenye vitongoji 90 kwenye majimbo ya mkoa huo, ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika na kusaidia vitongoji 740 vya mkoa huo vyote vinafikiwa".


"Niwaombe ndugu zangu REA na TANESCO msimamieni mkandarasi huyu afanye kazi kwa ubora kwani lengo la serikali kutoa fedha hizo ni kuhakisha huduma ya nishati inawafikiwa wananchi ambao wanauhitaji na huduma hiyo," alisisitiza Chongolo.


Mradi huo utanufaisha vitongoji 15 katika majibo yote ya mkoa wa Songwe ambayo ni Ileje, Momba, Tunduma,Mbozi,Vwawa na Songwe.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI