Header Ads Widget

TANROADS MBEYA YAANZA UTEKELEZAJI MRADI BARABARA YA ILEYA HAPOROTO ISHINDA.

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya umeanza kurekebisha barabara ya Ileya Haporoto Ishinda ambayo imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa maeneo hayo ya kata ya Ihango wilayani Mbeya.


Barabara hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kuwa ni mbovu licha ya umuhimu wake kwenye sekta ya usafiri na usafirishaji bidhaa mbalimbali.

Katika kutatua kero hiyo, Mhe. Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Oran Manasse Njeza, amefanya ziara katika kata ya Ihango ili kukutana na wananchi wake na kukagua miradi ya maendeleo ambapo wananchi wamekumbushia kero hiyo pamoja na nyinginezo katani humo.

Wananchi hao, wamesema barabara hiyo imekuwa mbovu lakini hazipitiki kwa urahisi hasa nyakati za kifuku ambapo wamemwomba Mbunge wao kuisukuma Serikali kutatua kero hiyo.


Akijibia kadhia hiyo, Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya Mhandisi Fransisco Mbaza, amesema tayari mkandarasi yuko eneo la mradi kwa ajili ujenzi wa makaravati na baadaye barabara kwani tayari imepasishwa hadhi kuhudumiwa na TANROADS.

"Ninayo furaha kuwaambia barabara yetu ya Haporoto Ishinda hadi Ileya imepasishwa hadhi kujengwa kwa kiwango bora kabisa cha TANROADS na tunamshukuru Mbunge wetu amepambana kupigania barabara hii", ameeleza Mhandisi Mbaza.


Naye Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amesema "Ndugu zangu tumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwasababu zimetoka hela zaidi ya million mia saba kwa ajili ya hii barabara yetu na wakandarasi nimekuja nao hapa na kazi imeshaanza kwa ajili ya barabara hii ambayo ilikuwa kero kweli", amesisitiza Mbunge Oran Njeza wa Mbeya vijijini.


Kuhusu kadhia ya maji kaimu meneja wa Wakala wa usambazaji maji vijijini RUWASA wilaya ya Mbeya Mhandisi Modestus Chingwile amesema RUWASA itashirikiana na  uongozi wa kata kuboresha vyanzo vilivyopo vya maji huku akitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji.

Amesema kata hiyo imekuwa na ongezeko la watu hivyo wakala huo utafanya jitihada za kutatua kero ya maji kwa wananchi wa vijiji mbalimbali ikiwemo Idimi na Haporoto.


Naye kaimu meneja wa shirika la umeme Tanzania TANESCO Mhandisi Godfrey Minzi amesema hivi karibuni watakwenda kufikisha nguzo tatu kwenye shule ya msingi Kawetere na kwenye zahanati.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI