Header Ads Widget

MWENYEKITI WA ACT WAZALENDO TAIFA OTHMAN MASOUD AKEMEA WANAOBEZA MATAKWA YA KATIBA

Na MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Act Wazalendo Othman Masoud Othman amesema wanaosema mabadiliko ya utawala hayawezi kubadilika Zanzibar kwa karatasi ya kura wanakwenda kinyume na masharti ya katiba ya Zanzibar ya  Mwaka 1984.


Othman Masoud aliyasema  hayo jana alipokuwa akifungua Kongamano la ngome ya Vijana lilofanyika katika ukumbi wa Jimbo la Ziwani,Wilaya ya Chake Chake Kusini Pemba.


Alisema baada ya mapinduzi mwaka 1964 nchi ilikuwa inaendeshwa kwa kutumia sheria zilizokuwa zikitungwa na kutekelezwa na baraza la Mapinduzi (DEGREE) kabla ya Rais wa Awamu ya Pili Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi kuamua mwaka 1979 Zanzibar kuandika Katiba yake ili kuimarisha msingi ya Demokrasia na Utawala Bora.

“leo anapotokea Mjinga Mmoja anasema hatutoi nchi kwa kikaratasi maana yake alie kuwepo ndio anatakuwepo tutarithishana sisi kwa sisi, Muulize anatokea nchi gani, wewe unatetea mapinduzi gani baada ya mapinduzi nchi iliendeshwa kwa Degree na mwaka 1979 nchi iliamua kutunga katiba,”


Alisema kwa mujibu wa katiba yam waka 1984 imesema Mapinduzi ya Zanzibar yataendelezwa kwa kutumia utaratibu uliolezwa kwa kwenye katiba ambapo msingi mmoja ni watu wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.


Akizungumzia suala la matumizi ya Fedha za Umma alisema Zanzibar haiwezi kupiga hatua ya maendeleo kama itakuwa na madeni makubwa ya mikopo kuliko mapato ambayo wanayakusanya kupitia vyanzo vya ndani.

Alisema  hivi sasa Zanzibar bajeti yake ya mwaka ni  Trilioni 1.5 wakati gharama za mishahara shilingi bilioni Mia Tisa na Shilingi Bilioni Mia Tatu unalipa Madeni.


“Sisi tunasema kutokana na haya nchi yetu imefikishwa kuendeshwa Shaghala baghala, wakati mwingine wakisema muwasikilize tuu lakini mimi siwezi kuwasikiliza kama kuharibu wao ndio wameharibu na wapinzani lengo lao kubwa kuona nchi inarekebishwa,” alisema.


Alisema ili Zanzibar ipige hatua za maendeleo kwa haraka ni lazima tuanzishe sheria zinazomheshimu Mwananchi kwa sababu Mwananchi ndio mfalme mbele ya Serikali.


Aidha Alisema Serikali haipaswI kufanya biashara badala yake inapaswa kusimamia sera na mipango kwa manufaa ya maendeleo ya Wananchi wake na iwapo Serikali ikifanya biashara itafika pahala nchi haiwezi kutawalika.


Othman ambae pia Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwanataalum Mkongwe wa Sheria alisema kama Serikali inataka kufanya biashara inapaswa kukata leseni badala ya kufanya biashara nyuma ya mgongo wa Serikali.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho Yusra Haji Kombo alisema Mabadiliko ya Utawala Zanzibar yanategemea nafasi kubwa ya Vijana na kuwakumbusha wengine umuhimu wa kufuatilia vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi ili waweze kukamilisha masharti ya kuandikishwa katika Daftari la kudumu la wapiga Kura Zanzibar.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, akifunga Kongamano hilo amesema, Chama hicho kina wajibu wa kuitumia rika ya vijana, hasa wale ambao wamepata mwamko na  kutamani kuleta mabadiliko ya kweli, kupitia Miongozo,  Elimu, na Msimamo thabiti wa  kupigania haki zao, pamoja na kuyafikia malengo ya kutetea Mamlaka Kamili ya Zanzibar.


Chama cha Act Wazalendo kinaendelea na mikutano ya ndani ya hadhara kisiwani pemba huku ikitumia mikutano hiyo kukosoa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar licha ya kuwa Sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI