Header Ads Widget

MOI YATAMBULISHA HUDUMA ZA KIDIGITAL, YAONYESHA UBOBEZI WA MATIBABU SABASABA

  


Na Matukio Daima Media 

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetambulisha mifumo ya kidijitali ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, huku ikionesha teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotumika katika matibabu ya kibingwa kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).


Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema ushiriki wa taasisi hiyo unalenga kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa, kutoa elimu kuhusu magonjwa ya mifupa na ubongo pamoja na kuonesha maendeleo ya teknolojia inayotumika katika utoaji wa huduma.


Amesema kuwa, MOI imejikita katika nguzo tatu kuu ambazo ni utoaji wa huduma za kibingwa, mafunzo kwa wataalamu wa afya wa ndani na kutoka nchi mbalimbali za Afrika, pamoja na kufanya tafiti zinazolenga kuboresha tiba kulingana na mazingira na vinasaba vya Waafrika.


Katika kuboresha huduma kwa wananchi, Dkt. Ulisubisya amesema taasisi hiyo imeanzisha mfumo wa kidijitali unaomwezesha mgonjwa kujisajili na kuweka miadi ya kuonana na daktari kupitia simu ya mkononi au kwa kutumia QR Code kabla ya kufika hospitalini.


Aidha, amesema hatua hiyo itapunguza misongamano na muda wa kusubiri huduma, huku ikiwarahisishia wananchi kupata huduma kwa wakati.


Mbali na huduma za ushauri na uchunguzi zinazotolewa katika banda la MOI, taasisi hiyo imeonesha matumizi ya teknolojia ya 3D Printing katika utengenezaji wa viungo bandia vinavyoendana na maumbo ya miili ya wagonjwa, ikiwemo mikono ya kisasa inayotumia betri.


Aidha, amesema MOI inaendelea kutumia mtambo wa kisasa wa Cathlab (Angio Suite) kutibu magonjwa ya mishipa ya damu ya ubongo, matatizo ya uti wa mgongo na kutoa tiba ya maumivu sugu kwa kutumia njia za kisasa zisizohitaji upasuaji mkubwa.


Katika maonesho hayo, baadhi ya wagonjwa waliowahi kutibiwa na taasisi hiyo walitoa ushuhuda wa mafanikio ya matibabu, akiwemo aliyesema alirejea kutembea baada ya kukaa kwa miaka minane bila uwezo huo.


Dkt. Ulisubisya amesema MOI pia inapanga kuanzisha kituo cha kudumu katika eneo la Sabasaba kitakachotoa huduma za awali kwa wananchi wa Mbagala, Mtoni na maeneo jirani, hatua itakayopunguza msongamano katika hospitali hiyo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI