Wakili wa kujitegemea na mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu kutoka mkoani Mbeya Ezekiel Mwampaka, amesema Serikali ndiye yenye dhamana kubwa ya kujibu hoja za wananchi kuhusu hali ya nchi kughubikwa na wimbi la watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Wakili Mwampaka amesema hayo wakati wa mahojiano yake maalum na kituo hiki ofisini kwake akitoa maoni kuhusu mwenendo wa nchi na hali ya usalama nchini.
Amesema hali ya Taifa la Tanzania hairidhishi kwa sasa kwani kumekuwa na vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa nchi hasa watu kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha huku familia zao zikisalia njiapanda.
Amesema Polisi ndiyo yenye wajibu wa kulinda raia na mali zao hivyo kuonyesha mashaka yake watu kupotea bila vyombo vya dola kutokuwa na taarifa.
"Watu wanapopotea tunatakiwa kuilaumu Serikali kwasababu mlinzi mkuu wa raia ni Polisi pamoja na mali zake. Raia anapopotea mtu wa kwanza kuulizwa ni Polisi, hata hapa Mbeya watu wanaripotiwa kupotea sio mara moja ni mara nyingi, kuna kijana wa Tukuyu (Shadrack Yusuph Chaula) hajulikani mpaka sasa yuko wapi japo tunasikia kuna mtu amempigia baba mzazi kutaka aweke million tatu ili kumpata kijana yaani mtu mpaka anapiga simu si wangeweza kumtafuta kwenye mfumo!", amehoji wakili Mwampaka.
Hata hivyo alipoulizwa matakwa ya kupatikana kwa katiba mpya, Mwanaharakati huyo amesema hilo ni hitaji muhimu katika kuleta uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.
"Mkwamo tulio nao mpaka sasa ni kwasababu ya Katiba tuliyo nayo. Katiba hii ina mamlaka makubwa kwa Rais wa nchi, ina mamlaka makubwa kwa Waziri na mamlaka hayo wanayatumia vibaya sasa tukipata katiba mpya kwanza itabidi tupunguze mamlaka ya Rais, kwamfano wewe ni Rais unaniteua mimi kuwa RPC wa mkoa wa Mbeya halafu anakuja aliyeniteua anasema hakikisha hapa fulani asipite, leo tumeambiwa tuna Tume huru ya Taifa ya uchaguzi hatuhitaji mabadiliko ya jina tunahitaji uhalisia wa Tume huru", ameeleza Wakili Ezekiel Mwampaka.
0 Comments