Header Ads Widget

WATU 12 WAFARIKI KWA AJALI TENA MKOANI MBEYA.

 


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Watu wapatao 12 wamefariki Dunia kwenye ajali ya gari iliyotokea ijumaa ya Septemba 06, 2024 katika kata ya Lwanjilo Halmashauri ya wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kwenda mkoani Tabora kuanguka.


Kwa mujibu wa jeshi la Polisi, mnamo Septemba 06, 2024 majira ya saa moja kuelekea saa mbili asubuhi huko katika eneo la Lwanjilo, Wilaya ya Mbeya katika barabara ya Mbeya  Chunya, Basi la abiria lenye namba za usajili T.282 CXT aina ya Yutong mali ya kampuni ya AN Classic lililokuwa likiendeshwa na Dereva Hamduni Nassoro Salum (37) Mkazi wa Tabora likitokea Mbeya kuelekea Tabora kupitia Wilaya ya Chunya liliacha njia na kwenda kugonga gema na kisha kupinduka na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa gari.


Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya ACP Wilbert Mica Siwa, amesema Katika ajali hiyo watu 12 wamepoteza maisha ambao ni wanaume 5 akiwemo aliyekuwa Dereva wa Basi hilo Hamduni Nassoro Salum, wanawake 7 miongoni mwao watoto wadogo ni wawili.


Kamanda Siwa amesema katika ajali hiyo watu 33 wamejeruhiwa ambao kati yao 22 ni wanaume na 11 ni wanawake na kwamba wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Kituo cha Afya Chalangwa kilichopo Wilaya ya Chunya.


Polisi mkoani Mbeya inasema uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu gari lake kwenye eneo lenye mteremko na kona kali hivyo kuendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI