Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI DANIEL SILLO APONGEZA KAMPUNI YA ASAS

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, Apongeza Kampuni ya Asas chini ya mkurugenzi wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Salim Abri Asas kwa Kudhamini  Maadhimisho ya wiki ya Mabalozi wa Usalama barabarani  kwa Miaka 6 sasa pamoja  na kutoa Bima ya Afya kwa Familia 50 Iringa .


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, ameipongeza kwa dhati Kampuni ya ASAS kwa kujitolea na kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha usalama barabarani.


 Akizungumza Leo  katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Iringa wakati wa maadhimisho ya Miaka  10 ya mabalozi wa usalama barabarani nchini  alisema kuwa kampuni hiyo ya Asas  ambayo ni mdhamini mkuu ni jambo jema ambalo lina umuhimu mkubwa katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kufuata sheria za barabarani na kuchukua hatua stahiki za kujikinga na ajali.

 Naibu Waziri Sillo alisisitiza kuwa usalama barabarani ni suala linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.

 Alieleza kuwa ni jambo la kufurahisha kuona kampuni kama Asas zikijitoa kwa hali na mali kusaidia juhudi hizi muhimu, ambazo zina lengo la kupunguza ajali na vifo barabarani ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa changamoto kubwa kwa taifa.

Alisema kuwa kampuni ya Asas  haikuishia tu kudhamini maadhimisho hayo, bali pia ilichukua jukumu la kusaidia jamii kwa kutoa bima ya afya kwa familia 50 ambazo zina mahitaji maalum.

" Hatua hii ya kipekee ni ishara ya ushirikiano wenye tija kati ya sekta binafsi na serikali, ikiwa na lengo la kuboresha ustawi wa wananchi, hususani familia ambazo haziwezi kumudu gharama za huduma za afya"

Naibu Waziri Sillo aliipongeza Asas  kwa hatua hiyo muhimu ya kusaidia familia zisizojiweza, akisema kwamba hatua hiyo inakwenda sambamba na juhudi za serikali za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa urahisi kwa wananchi wote. 

Hivyo aliwataka wadau wengine wa sekta binafsi kuiga mfano wa Asas kwa kushiriki kikamilifu katika kusaidia kutatua changamoto za kijamii, hususani katika nyanja za afya na usalama barabarani.


Kuhusu mabalozi hao wa usalama barabarani alisema kuwa mabalozi hao wanaliongezea nguvu jeshi la polisi na ni sawa na polisi jamii na sio kuchukua nafasi za askari wa usalama barabarani .

Alisema mabalozi wa usalama barabarani ni sehemu ya mpango wa kitaifa uliolenga kuelimisha wananchi kuhusu mbinu bora za kuepuka ajali na kuboresha utendaji wa madereva, abiria, na watumiaji wa barabara kwa ujumla. 

Hivyo kwa kupitia mabalozi hawa, elimu hutolewa kuhusu masuala kama vile umuhimu wa kuvaa mikanda ya usalama, kufuata alama za barabarani, na kuepuka uendeshaji wa kasi.

Akielezea umuhimu wa mabalozi wa usalama barabarani, Naibu Waziri Sillo alisema kuwa hawa ni watu wenye dhamira ya dhati ya kuona mabadiliko katika utamaduni wa matumizi ya barabara.

 Aliwahimiza mabalozi hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa moyo mmoja ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaopoteza maisha au kupata majeraha mabaya kutokana na ajali za barabarani.

 Naibu Waziri alibainisha kuwa mchango wa sekta binafsi ni muhimu sana katika kusaidia kampeni za serikali za kuboresha usalama barabarani. Alisema kuwa serikali pekee haiwezi kufikia malengo ya kupunguza ajali za barabarani bila kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo kampuni kama Asas , ambazo zimekuwa zikitoa msaada mkubwa katika maeneo mbalimbali ya kijamii.

Katika hatua nyingine alisema wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho katika kukamilisha maboresho ya sheria za usalama za barabarani kisha kufikishwa bungeni ili sheria hizo zibadilishwe na kuendana na wakati.

Waziri Sillo, alisema elimu ya usalama barabarani ndiyo Nyenzo muhimu katika kutokomeza matukio ya ajali kwani kwa aslimia kubwa zimeonekana zinatokana kuwa ni za makosa ya kibinadamu.

Aidha ameelezea kauli mbiu ya mwaka huu inayo sema "ushirikishwaji wa wanawake katika kuimarisha usalama barabarani ni nyenzo muhimu katika kuokoa maisha" na kuongeza kuwa kauli hiyo inatoa changamoto ya kupanua wigo wa elimu zaidi kutokana na waathirika wengi wa ajali hizo kuwa wanawake na watoto.

Mkuu wa wilaya ya Iringa, Kheri James, ambaye amemuwakilisha mkuu wa mkoa huo, Peter Serukamba, alishukuru shughuli hiyo kufanyika katika mkoa huo, pamoja na kuahidi kuendeleza ushirikiano pamoja na jeshi la polisi ili kuendelea kudhibiti ajali za barabarani.


Kwa upande wake mwakilishi wa kamanda wa usalama barabarani Ramadhani Ng'anzi Kamishana msaidizi wa polisi na CEO wa elimu na mafunzo ya usalama barabarani kwa umma, Michael Deleli, alisema jeshi hilo limeendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kupanua wigo wa kuweka polisi kata kila eneo ili kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila mtu.

Kamanda Deleli alisema makosa ya usalam barabarani yamegawanyika katika makundi matatu ikiwemo, Makosa ya kibinadamu ambayo kwa asilimia 75 yanachangia ajali zote za barabaarani, Ubovu wa vyombo vya moto asilimia 25 pamoja na ubovu wa miundombinu, hivyo elimu inahitajika zaidi ili kutokomeza makosa hayo.

Awali akisoma risala ya taasisi yao, Mkurugenzi mtendaji wa bodi ya mabalozi wa usalama barabarni (RSA) Tanzania, Augustus Fungo, alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii juu ya usalama barabarani kwa zaidi ya miaka 10 (10), kuripoti matukio ya ajali na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani pamoja na  kushawishi serikali juu mabadiliko ya sheria na sera za usalama barabarani.

Fungo, aliomba serikali kuangali upya sheria za usalama barabarani na kuzibadilisha kwani zimepitwa na wakati na kupelekea makosa ya barabarani kuendelea kuongeza kutokana na baadhi ya madereva kutokuwa na wasiwasi na sheria hizo.

"Eneo lingine linalotukwamisha ni eneo la mabadiliko la sheria za usalama barabarani, Mheshimiwa Mgeni rasmi, sheria hizi ni za zamani sana, na katika kila RSA day tumekuwa tukijaribu sana kukumbishia mara kwa mara, kwamba tunahitaji kubadili sheria za barabarabi kwa sababu ni za zamani na zina faini mpaka ya shilingi 1000" alisema Fungo.


Huku MNEC Asas ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoa wa Iringa alisema kuwa kampuni yake  imekuwa ikiunga mkono shughuli mbalimbali za kijamii kama sehemu ya jukumu lake kwa jamii, na itaendelea kushirikiana na serikali katika masuala muhimu kama usalama barabarani na huduma za afya. 

Mnec  Abri, alitaka kila mmoja kuwa balozi wa mwenzake katika kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua na hatimae kuisha kabisa.

"Nataka nijalilize katika shukrani, tumeshukuriwa kwamba miongoni mwa wadhani wanaodhamini  shughuli za hawa ndugu zetu mabalozi na hasa elimu ya usalama barabarani, mimi kwa mtazamo wangu, na wengi mtakubaliana nami, hawa mabalozi endapo watu wangejua thamani ya hawa mabalozi na fikiri kila taasisi, kila NGO's ndani ya taasisi wanatakiwa wawe mabalozi au wananchama, tumepata kushuhudia ndani ya nchi yetu historia tumewahi kupoteza waziri mkuu ajali ya barabaraniTanzani, tumewahi kupoteza manaibu waziri, tumewahi kupoteza naibu Waziri Salome Mbatia mimi nakumbuka hapa Iringa alifia Njombe huko, tumepoteza maprofesa, tumepoteza madaktari, tumepoteza wanataaluma mbalimbali kwa hizi ajali barabarani, tumepoteza mpaka maiti, unasikia maiti inasafirishwa sehemu moja kwenda mfano inatoka Mbeya labda inapelekwa mkoa flani waliokuwepo kwenye gari wamekugfa na maiti imekufa tena"

"Kufa ni kufa kwa bahati mbaya tumekuwa tukiweka viwango vya kufa, hivi sisi tukienda kule kwenye makaburi yamewekwa kwa viwango yaani, huyu amekufa kwa ajali huyu amekufa ukimwi huyu amekufa kwa maradhi, kufa ni kufa kwanini akifa mwanasiasa mmoja nchi nzima inatikisika lakini wanaokufa kwa ajali tunanyamaza, kwanini, tuwapiganie hata wale wanaokufa kwa ajali hizi za barabaarani, nawapongeza sana RSA, ninyi ni watu wa maana sana ndani ya nchi hii, gari limebeba mgonjwa , linakwenda kuchukua mgonjwa linapata ajali mgonjwa na dereva wanakufa wote"

"Nani ambaye hatumii vyombo vya moto ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, hayupo hivyo ji jukumu letu kuhakikisha tuakwenda kuachana na ajali hizi, nawapongeza sana RSA mmekuwa mabalozi wazuri " alisema Asasi


kamanda wa polisi mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi, amesema mkoa huo umeendelea kuwa salama katika nyanja zote ikiwemo upande wa ajali za barabarani huku akipongeza kampuni ya Asas pamoja na Mnec Salim Abri kwa endelea kuwa mstari wambele katika mapambano ya ulinzi na usalama kwa mkoa huo.


Alisisitiza kuwa kampuni yao inaamini katika kujenga jamii salama na yenye afya bora, na ndiyo sababu wameamua kusaidia familia hizo 50 kwa bima ya afya.


Wanufaika wa bima hizo za Afya kutoka kampuni ya Asas Wamepongeza kampuni hiyo kwa msaada huo.

 

CHINI MATUKIO KATIKA PICHA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA MABALOZI WA USALAMA BARABARANI KITAIFA MKOANI IRINGA.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI