Msanii maarufu wa muziki, Emmanuel Elibariki anayefahamika kama Nay wa Mitego, anakabiliwa na mashtaka ya ukiukwaji wa kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kufuatia kutoa wimbo wake mpya "NITASEMA" mnamo tarehe 24 Septemba 2024 bila kibali. Baraza limeainisha makosa manne yanayomkabili msanii huyo kama ifuatavyo:
Kosa la Kwanza: Kutoa Wimbo Bila Kibali
Kwa mujibu wa Kanuni ya 25(1) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, 2018, Nay wa Mitego alitoa wimbo wake kwa walaji kabla ya kupata kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui ya wimbo huo yamezingatia maadili. Wimbo huo ulisambazwa bila kufuata taratibu stahiki, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kosa la Pili: Maudhui Yenye Uchochezi
Wimbo huo pia unadaiwa kuwa na maudhui ya kichochezi, jambo linalokwenda kinyume na Kanuni ya 25(6)(d) ya Kanuni za BASATA. Mashairi ya wimbo yanadaiwa kuhamasisha vitendo vya uchochezi dhidi ya Serikali, huku ukidai kwamba Serikali inahusika katika vitendo vya utekaji na mauaji ya watu.
Kosa la Tatu: Kupotosha Jamii
Mashairi ya wimbo "NITASEMA" yanadaiwa kupotosha umma kwa kudai kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshindwa kutekeleza majukumu yake, na kwamba miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake imetelekezwa. Hili limekiuka Kanuni ya 25(6)(b) ya Kanuni za BASATA.
Kosa la Nne: Kukashifu Mataifa Mengine
Katika wimbo huo, Nay wa Mitego anadaiwa kutoa matamshi yanayokashifu mataifa ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jambo linaloweza kusababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi hizo. Hii inakwenda kinyume na Kanuni ya 25(6)(h) ya Kanuni za BASATA.
Kutokana na makosa haya, Baraza la Sanaa la Taifa linamtaka msanii huyo kufuata sheria na taratibu zinazohusu usambazaji wa kazi za sanaa nchini. Hatua zaidi za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yake ikiwa atapatikana na hatia ya makosa yaliyotajwa.
E.E. Buganga Katibu Mtendaji, BASATA
Nakala: Katibu Mtendaji, kwa kumbukumbu
0 Comments