Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MADIWANI katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji wameutaka oungozi wa halmashauri hiyo kuwasilisha taarifa za miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri hiyo ili waweze kujua na kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo inayoendelea kwenye halmashauri yao.
Kauli hiyo ya madiwani imetolewa kwenye kikao cha robo ya nne ya baraza la madiwani la halmashauri hiyo ambapo madiwani walilalamikia kutokuwepo kwa taarifa za utekelezaji wa mpango wa kutoa elimu ya ukimwi katika mradi wa uboreshaji miji kiushindani Tanzania (TACTIC).
Naibu Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mgeni Kakolwa ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya baraza la madiwani la halmashauri hiyo alisema kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo wa TACTIC hakuna taarifa za elimu na afua za ukimwi ambazo kamati yake imepokea na kuzijadili.
Sambamba na hilo Naibu Meya huyo alisema kuwa kwenye mpango wa utekelezaji na bajeti kipengele hicho kipo na kimetengewa fedha hivyo walipaswa kujua na kutembelea kuona maendeleo ya utoaji elimu jambo ambalo halifanyiki nay eye binafsi kuwa Mwenyekiti hewa wa kamati hiyo.
Diwani wa kata ya Businde, Masudi Kassim akizungumzia jambo hilo alisema kuwa mradi huo una muda sasa unatekelezwa na hii ni awamu ya pili hivyo Mkurugenzi anapaswa kuwa na majibu ya wapi taarifa hizo zinakwama kupatikana na kuwasilishwa kwenye baraza hivyo madiwani wamemtaka Mkurugenzi huyo kutafuta taarifa hizo na kuleta kwenye vikao vya baraza.
Akizungumza kwenye kikao hicho cha baraza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kisena Mabuba alisema kuwa amelisikia jambo hilo likizungumzwa mara nyingi nje ya vikao vya baraza likionekana kuwa na maslahi binafsi ya madiwani na kuwataka madiwani kufuata kanuni na taratibu za vikao katika kuleta hoja zao ili kusiwe na mgongano wa maslahi.
Akifunga hoja hiyo Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji akiwa Katibu wa Baraza hilo la madiwani kutafuta taarifa hizo lakini pia kutafuta mwongozo na taratibu ambao utawezesha kamati ya kudumu ya ukimwi ya baraza hilo la madiwani kufupata taarifa hizo na kukagua utekelezaji wake.
0 Comments