Header Ads Widget

MAKALA:MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA NI DHAHABU YA UTALII KUSINI.

 



NA FRANCIS GODWIN,IRINGA 

UTALII ni Moja kati ya dhahabu inayopatikana kwa urahisi zaidi ndani ya 
Taifa la Tanzania kwani ni mgodi unaoingiza kipato kwa Kila mmoja hata bila kuchafuka na vumbi kama ilivyo kwa wachimbaji wa dhahabu yenyewe.

Sekta hii ya utalii imekuwa ikiingiza Pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla iwapo Kila mmoja Wetu atahitaji kuwa sehemu ya utalii .

Faida ya utalii kwa mikoa ya kaskazin mwa Tanzania si za kujiuliza Wala kutafuta maana Vizazi vyote vya mikoa hiyo vimerithishwa utalii na vinapenda utalii na ndio maana utalii huko umekuwa mkubwa zaidi .


Sitaki kuzungumzia sana sababu za kukua kwa sekta ya utalii wa mikoa ya kaskazin kwa Leo ila niseme tu Miundo mbinu Bora imechangia ukuaji wa sekta hii ya utalii huko.

Kutokana na ukuaji huo wa utalii mikoa hiyo mkoa wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu kusini haipo nyuma kuendelea kuvutia watalii hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Jitihada hizo zimeanza kuonekana baada ya kuwepo kwa wazo na sasa kuanzisha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni Fursa za Kiuchumi kwa Wananchi na Taifa pia uungaji mkono jitihada za Rais Dkt Samia  Suluhu Hassan katika Kukuza Utalii Kupitia The Royal Tour.


Mwaka 2024 unashuhudia maadhimisho makubwa ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, moja ya hifadhi kubwa na maarufu zaidi barani Afrika.

 Maadhimisho haya yatakayofanyika kuanzia Oktoba 1 hadi 7, 2024, ni fursa muhimu kwa Watanzania kusherehekea mafanikio ya uhifadhi, kujifunza kuhusu umuhimu wa maliasili, na kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utalii.


Katika kilele cha maadhimisho haya, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. 

Hafla hiyo itahusisha uzinduzi wa huduma mpya za kitalii, zikiwemo utalii wa puto ambao utawapa watalii fursa ya kuona mandhari ya kuvutia ya Hifadhi ya Ruaha kutoka angani.

 Hii ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuongeza vivutio vya utalii na kuvutia wageni zaidi. 

Pamoja na matukio haya ya kitalii, maadhimisho hayo yatahudhuriwa na viongozi wa kimila na dini kutoka mkoa wa Iringa, na kutakuwa na mijadala maalum juu ya mafanikio, changamoto, na njia bora za kuimarisha uhifadhi wa maliasili.


Ikumbukwe Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inatoa mchango mkubwa kwa uchumi wa mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla. 

Pia eneo hili la kitalii limekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa wenyeji wa Iringa, ambao wengi wao wanajihusisha na sekta ya utalii kwa njia tofauti. 

Wakazi wanapata ajira kupitia uongozi wa watalii, huduma za malazi, migahawa, na biashara za kitalii kama vile utengenezaji na uuzaji wa bidhaa za sanaa na ukumbusho. 

Katika kipindi cha maadhimisho haya, shughuli nyingi za kijamii na kibiashara zimepangwa ili kuimarisha uhusiano kati ya hifadhi na jamii za jirani.

Uzinduzi wa utalii wa puto ni fursa nyingine muhimu kwa wananchi wa Iringa. 

Huduma hii mpya inatarajiwa kuvutia idadi kubwa ya watalii wa kimataifa na ndani, na hivyo kuimarisha zaidi sekta ya utalii mkoani humo.

 Hivyo hali hii itachochea ongezeko la biashara ndogo ndogo, ujenzi wa miundombinu ya malazi kama vile hoteli na nyumba za wageni, pamoja na kuimarisha huduma za usafiri kama vile taksi na magari ya kitalii.

Mbali na kuimarisha ajira na biashara, miundombinu ya mkoa wa Iringa nayo inaboreshwa kwa ajili ya kusaidia utalii.

 Barabara ya lami ya kilomita 104 kutoka Iringa mjini hadi Msembe, ambayo ni lango kuu la Hifadhi ya Ruaha, imekuwa ikiboreshwa ili kurahisisha usafiri. 
Pia, uwanja wa ndege wa Iringa uko mbioni kukamilika, hatua ambayo itapunguza muda wa safari kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, hivyo kuongeza idadi ya wageni. 

Hatua hizi zote zinawawezesha wananchi wa Iringa kunufaika kiuchumi kupitia sekta ya utalii, na hivyo kuinua kipato chao na kuboresha hali zao za maisha.

Katika kipindi cha maadhimisho haya, jamii za jirani, wakiwemo watu wenye ulemavu na familia zinazoishi kwenye mazingira magumu, zitapatiwa msaada maalum. 

Hii ni sehemu ya jitihada za Hifadhi ya Ruaha kuimarisha uhusiano na jamii za jirani kwa lengo la kuonyesha umuhimu wa uhifadhi wa maliasili na faida zake za kiuchumi kwa watu wa kawaida.


 Watoto na vijana pia watahusishwa kwenye shughuli za kijamii na elimu juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira, hatua ambayo itachangia kuandaa kizazi kipya chenye mwamko wa uhifadhi.

Hata hivyo mbali na mchango wake kwa mkoa wa Iringa, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa zima.

 Utalii unachangia sehemu kubwa ya pato la taifa kupitia ada mbalimbali zinazolipwa na wageni wanaotembelea hifadhi, ikiwemo ada za kuingia, malazi, na huduma nyingine za kitalii. 

Hifadhi ya Ruaha ni maarufu duniani kutokana na ukubwa wake, aina mbalimbali za wanyama, na mandhari ya kuvutia. Inaelezwa kuwa hifadhi hii ni makazi ya idadi kubwa ya tembo wapatao 15,000, nyati 20,000, na zaidi ya simba 8,000.

 Hali hii inafanya Ruaha kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje, hivyo kuingiza mapato makubwa ya kigeni.

Utalii pia una mchango mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya nchi. 

Ukarabati wa barabara, uwanja wa ndege wa Iringa, na miundombinu ya ndani ya hifadhi kama vile kambi za wageni na maeneo ya mapokezi umeongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wageni. Hii siyo tu inaongeza idadi ya watalii, bali pia inasaidia kuongeza mapato yanayopatikana kutoka kwenye huduma za kitalii.

Zaidi ya hayo, Hifadhi ya Ruaha inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye nishati ya taifa kupitia Mto Ruaha, unaopitia ndani ya hifadhi hiyo. 

Mto huo ni chanzo muhimu cha maji kwa bwawa la Mtera, ambalo linazalisha umeme unaotegemewa na taifa. 
Kwa hivyo, uhifadhi wa mto huo ni muhimu siyo tu kwa mazingira, bali pia kwa uchumi wa taifa ambao unategemea nishati ya umeme kwa shughuli za viwanda na maendeleo mengine.

Mbali na mchango wake kwenye uzalishaji wa umeme, Hifadhi ya Ruaha pia inachangia kwenye mapato ya kigeni kwa kuvutia watalii wengi wa kimataifa. Watalii hawa wanalipa ada mbalimbali, kununua bidhaa na huduma, na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia utalii endelevu.

Zimekuwepo jitihada za Rais Dkt Samia kukuza na kutangaza utalii  Kupitia filamu ya The Royal Tour hakuna ubishi Katika jitihada za kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kupitia mpango wa kimataifa unaojulikana kama The Royal Tour. 


Kwani huu ni mradi maalum uliolenga kuhamasisha na kutangaza vivutio vya kiutalii vya Tanzania kwa soko la kimataifa.

 Kupitia filamu ya The Royal Tour, Rais Samia alichukua jukumu la kuwa mwongoza watalii, akitembea na kuonyesha maeneo mbalimbali ya kihistoria, kitalii, na kitamaduni yanayopatikana nchini Tanzania.

Filamu hiyo imepokelewa vizuri kwenye majukwaa ya kimataifa na imechangia kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.

 Watalii hawa wanavutiwa na vivutio vya kipekee vilivyopo Tanzania, vikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na Zanzibar. 

Mafanikio ya The Royal Tour yameongeza mwonekano wa Tanzania kwenye ramani ya utalii duniani, na hivyo kuongeza idadi ya wageni wanaokuja kutalii nchini.

Mbali na watalii wa kimataifa, The Royal Tour pia imechangia kuongeza mwamko wa utalii wa ndani. 

Watanzania wengi sasa wameanza kuthamini na kutembelea vivutio vya ndani, jambo ambalo limesaidia kuongeza pato la taifa kupitia utalii wa ndani.

 Rais Samia amesisitiza umuhimu wa Watanzania kufahamu na kuthamini urithi wao wa asili, na hii imepelekea kuongezeka kwa utalii wa ndani, hasa miongoni mwa vijana.

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inafaidika moja kwa moja kutokana na jitihada hizi za Rais Samia. 

Kupitia mpango wa The Royal Tour, hifadhi hii imepata umaarufu zaidi duniani, na idadi ya watalii inatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka michache ijayo. 

Mafanikio haya ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa serikali wa kuhakikisha kwamba utalii unakuwa sekta kuu ya kuchangia uchumi wa taifa, na kuimarisha mapato ya kigeni.



Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwel Ole Meing’ataki anasema  maandalizi ya maadhimisho hayo yatatanguliwa  na shughuli mbali mbali za kijamii pamoja na elimu juu ya umuhimu wa Hifadhi hiyo.

Anasema kuwa Hifadhi imejipanga kuimarisha uhusiano na jamii mbalimbali, ikiwemo watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuwapatia fursa ya kutembelea hifadhi hiyo pamoja na kutoa msaada kwa familia zenye mazingira magumu

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote, hususan wakazi wa Iringa, katika maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Oktoba, 2024, huku kilele chake kikitarajiwa kuwa tarehe saba,” alisema Meing’ataki.

Kuwa  mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo Balozi Dkt. Chama  ambaye atahitimisha shughuli hiyo kwa kuzindua rasmi utalii wa puto. 

Kuwa huduma hii mpya ya utalii wa puto inalenga kuwavutia watalii zaidi katika hifadhi hiyo kwa kuwapa fursa ya kufurahia mandhari ya kuvutia ya Ruaha kutoka angani.

Alisema Katika maadhimisho hayo, Hifadhi ya Ruaha itashirikiana na wadau mbalimbali wa mkoa wa Iringa, wakiwemo viongozi wa kimila na kidini, kwa kufanya ziara maalumu za kutembelea hifadhi hiyo. 

Meing’ataki anaeleza kuwa ziara maalum kwa Chifu wa kabila la Wahehe na viongozi wake wa kimila, pamoja na viongozi wa dini, zimepangwa ili kuongeza uelewa na ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira.

Pia, alisema kutakuwa na kongamano maalum la miaka 60 ambalo litajikita katika kujadili historia ya hifadhi hiyo, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo, sambamba na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha uhifadhi.

Hifadhi hiyo pia imeandaa ziara kwa watu wenye ulemavu kutoka mkoa wa Iringa ili wapate fursa ya kutembelea na kujionea vivutio vilivyomo katika hifadhi ya Ruaha.

 Aidha, wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo, hasa wenye mazingira magumu, watapewa msaada na kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maliasili na faida za kiuchumi zinazoweza kupatikana kutokana na utalii endelevu.

Katika hatua nyingine, Meing’ataki amebainisha kuwa kutakuwa na bonanza la michezo litakalofanyika katika eneo la Tungamalenga kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi kupitia burudani.


Meing’ataki anasema kuwa maboresho makubwa yamefanyika katika miundombinu ya hifadhi hiyo, ikiwemo maeneo ya mapokezi, malazi, na barabara, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Mbali na kuwa kivutio kikubwa cha watalii, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pia ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. 

Mto wa Ruaha, ambao unapita ndani ya hifadhi hiyo, ni chanzo muhimu cha maji kwa bwawa la Mtera, ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa umeme nchini.

 Hivyo uhifadhi wa mto huo unasaidia kuhakikisha uzalishaji endelevu wa nishati ya umeme ambayo inategemewa na taifa.

Hifadhi ya Ruaha pia inachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya kigeni kupitia utalii.

Kuwa  watalii wanaotembelea hifadhi hiyo hulipa ada mbalimbali za kuingia, malazi, na huduma nyinginezo, ambazo huingiza mapato makubwa kwa taifa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Iringa mjini Frank Nyalusi alisema maadhimisho hayo yatafungua fursa kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Iringa hivyo hawana budi kuchangamkia fursa za kiutalii.

Anasema tayari ujenzi wa Barabara ya lami Kilomita 104 toka Iringa mjini Hadi Msembe katika lango la Hifadhi hiyo inajengwa pia Uwanja wa Ndege wa Iringa upo Mbioni kumalizika kuwa itachangia kukuwa kwa utalii.

Huku muongoza watalii Salafino Lanzi akieleza kuwa maadhimisho hayo ni fursa kwao kwani idadi ya watalii itaongezeka zaidi .

Maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yanaashiria hatua kubwa zilizopigwa katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini hivyo no wakati muafaka kwa Watanzania wote kushiriki katika juhudi za kuendeleza na kulinda urithi wa asili wa nchi yetu kwa vizazi vijavyo.


Hifadhi hii imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya utalii, uchumi wa taifa, na maendeleo ya jamii za jirani.

 Huduma mpya za kitalii kama utalii wa puto, uboreshaji wa miundombinu, na jitihada za Rais Samia ndio maana nalazimika kusema "MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA NI DHAHABU YA UTALII KUSINI"


KWA HABARI NA MAKALA MBALI MBALI ENDELEA KUFUATILIA MATUKIO DAIMA APP,MATUKIO DAIMA BLOG NA MATUKIO DAIMA TV (ONLINE) PIA MITANDAO YOTE YA KIJAMII NA USIKOSE KUSOMA GAZETI LA MWANAHABARI NA MACHINGA KILA SIKU IWAPO UNAHITAJI KUTANGAZA NASI PIGA SIMU 0754026299 EMAIL: matukiodaima3@gmail.com

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI