Na Matukio Daima App, Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali ,Maulid Surumbu amesema serikali inatambua changamoto za wazee ikiwemo jamii kushindwa kuwaheshimu ,kuwaumiza na kukosa haki zao za msingi baada ya kustaafu.
Kanali ,Surumbu amesema leo Septemba 27 mwaka huu wakati amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera kwenye Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ruanda Nzovwe Jijini hapa.
Amesema kuwa ni mambo ambayo yanaleta fedhehea ya kiutu huku ikitawaliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba wazee hao wamewalea kwa upendo, uvumilivu ,hali ngumu bila kukata tamaa pamoja na kuwaendeleza mpaka kufikia hatua walizofikia.
Hata hivyo Kanali Surumbu amesema serikali inatambua asilimia kubwa ya wazee wanalea watoto yatima na wasiojiweza pamoja na waliotelekezwa.
Akizungumzia kuhusu mabaraza ya ushauri ya wazee,amesema yamekuwa msaada katika kusuluhisha migogoro na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili hivyo ni wajibu kuhakikisha yanakuwa na vikao kwa mujibu wa mwongozo wa kupokea na kujadili taarifa zake
Aidha Kanali Surumbu amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,Mkoa wa Mbeya una wazee 2,343,754 ambapo kati yao wanawake ni 1,219,926 , wanaume 1,123,828 hivyo idadi ya wazee kuwa asilimia 5.9 ya wakazi wa mkoa Mbeya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la wazee mkoa wa Mbeya ,Arthur Mwankenja amesema bado kuna mambo ambayo yamekuwa yakiathiri ustawi wa huduma kwa wazee ikiwemo watumishi waliostaafu kazi serikalini kutopata mkupuo wa pensheni zao na pia baada ya kupitishwa kikotoo wapo watumishi ambao walitumikia umma kwa zaidi ya miaka 30 lakini huambulia mkupuo wa mil.23 na wengine mil.8 pekee.
Mwankenja pia amesema malipo ya pensheni jamii kwa wazee ambao hawakuwa watumishi wa serikali kama ilivyo Zanzibar wameomba wazee kuanzia miaka 70,ombi hilo lifanyiwe kazi ili kuwaondolea adha wazee hao.
"Tunaomba serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ilifabyie kazi suala hili ili na sisi tuwe kama wenzetu wa Zanzibar wanaopata pensheni tunaamini kupitia baraza hili la wazee tutafikiriwa "amesema
Maadhimisho ya siku ya wazee Dunini kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Tabora October Mosi mwaka huu huku Kauli mbiu ya siku ya wazee ikisema "Tuimarishe huduma kwa wazee, wazeeke kwa heshima
0 Comments