Header Ads Widget

MWALIMU ATUPWA MIAKA 30 JELA KWA KUMNAJISI MTOTO WA MIAKA 13 WILAYANI KYELA .




NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, imemhukumu mwalimu Juma Venance Mhanga (41) mkazi wa kata ya Njisi kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumnajisi binti mdogo mwenye umri wa miaka 13 mwanafunzi wa shule moja ya sekondari wilayani Kyela.


Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi Paul Barnabas Mabula wa mahakama ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wakati akisoma hukumu kwenye shauri ubakaji ambalo mwalimu huyo wa shule ya msingi alikuwa akishtakiwa nalo.


Hakimu Mabula amesema mahakama yake imeridhika bila kuacha shaka kwamba mara kadhaa mshtakiwa Juma Venance Mhanga alimwingilia kimwili mwanafunzi huyo ambaye anaishi na bibi yake wilayani Kyela.



Amesema kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili yaani Jamuhuri na utetezi bado ameridhika na maelezo ya upande wa Jamuhuri ambao haujatikiswa hata kidogo na hoja za mshtakiwa kukana kutenda kosa la ubakaji wa mtoto huyo.


Amesema hata wakati wa uwasilishaji ushahidi wa upande wa mashtaka, shahidi muhimu ambaye ni mhanga alifika mahakamani na kueleza kuwa mara kadhaa mwalimu huyo aliyezoeana na bibi yake na ni majirani alikuwa akienda kuchaji simu na kuangalia mpira nyumbani kwao kutokana na nyumba yake kutokuwa na umeme hivyo amekuwa akimbaka bibi yake akiwa hayupo na kumuonya kutosema kwani bibi yake angemfukuza nyumbani hapo hadi alipoamua kusema baadaye.


Mwanafunzi huyo anadaiwa kuwa mara kadhaa na ghafla alianza kuonekana na vyakula kama maandazi na biscuit shuleni hivyo kudhaniwa anamuibia bibi yake ambaye ni mjasiriamali lakini alipoulizwa alidai amekuwa akipewa na mwalimu huyo akimtaja kama mpenzi wake na siku moja baada ya kufika nyumbani kwao aliingia hadi chumbani na kumbaka mtoto huyo kisha kumpatia fedha shilingi 1500 hali iliyomsababishia maumivu.


Pia mashahidi wengine sita walifika mahakamani kutoa ushahidi wao akiwemo daktari aliyemchunguza binti baada ya kubakwa pamoja na mwalimu wa shule ya msingi aliyokuwa akifundisha mwalimu huyo ambaye alieleza kuwa mwalimu huyo hana mahudhurio mazuri shuleni na hivyo pia ana shauri la kinidhamu shuleni hapo.


Kwenye utetezi wake mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo bali alidai kuwa bibi wa mhanga ndiye amekuwa akimtaka kimapenzi hivyo baada ya kumkatalia ndipo wamemuundia kesi hiyo huku pia akidai kwakuwa ni mgonjwa wa mkono siku moja kabla ya tarehe ya tukio alinunua dawa za maumivu hivyo asingeweza kutekeleza tukio la ubakaji ambalo linahitaji matumizi ya nguvu.


Pamoja na hayo, Mahakama imesema imeridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka ambao una uzito hivyo kumtia hatiani mwalimu Mhanga ambapo wakili wa Serikali Davice Msanga aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa mtumishi huyo ambaye alipaswa kuwa kioo cha jamii, mlezi wa watoto na kwamba aliaminiwa na bibi wa mhanga hata kuwa huru na makazi yake hata asipokuwepo.


Mshtakiwa alionekana mwenye kujiamini mahakamani hapo huku akisisitiza hakufanya kitendo hicho kwani hata Mungu anajua kuwa hakufanya baadaye akaiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni mgonjwa na hawezi kufanya kazi ngumu.


Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Kyela Paul Mabula amemhukumu mwalimu Juma Venance Mhanga (41) kwenda jela miaka 30, kumlipa mhanga fedha kiasi cha shilingi laki tano kama fidia pamoja na kuchapwa fimbo nne.


Baada ya Mahakama kumalizika bibi wa mhanga ameishukuru mahakama na wadau kwa maelezo kuwa mahakama imetenda haki.


Mwendesha mashtaka wa Serikali Davice Msanga ambaye pia ndiye mkuu wa mashtaka wilaya ya Kyela amesema upande wa Jamuhuri umeridhika na maamuzi ya mahakama na kuitaka jamii hasa wazazi na walezi kuwa makini kwa kuangalia watoto ili kuwalinda dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili, ubakaji, ulawiti na unyanyasaji kwa ujumla wake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI