NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WAKAZI wa kijiji cha Sembeti kata ya Marangu Mashariki Jimbo la Vunjo, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha kijiji hicho na kijiji jirani cha Samanga lililoanza ujenzi miaka 18 iliyopita kwa gharama ya shilingi milioni 103.5
Wametoa pongezi hizo mbele ya Mbunge wa jimbo la Vunjo Dkt Charles Stephen Kimei aliyetembelea kijiji hicho kukagua na kuhamasisha kazi za maendeleo sambamba na kusikiliza kero za wananchi.
Wamesema, kukamilishwa kwa daraja hilo la Sembeti - Samanga kutachochea uchumi wa vijiji hivyo na kutaimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwani litaondoa kabisa gharama za ziada katika uvushaji vitu mbalimbali ikiwemo bidhaa na vitu vya biashara au vifaa vya ujenzi kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Akihutubia Mkutano huo Mbunge Dkt Kimei amesema kukamilishwa kwa daraja hilo ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inathamani maisha ya wananchi na kuwataka wananchi kulitumia daraja hilo kuchochea na kuongeza shughuli za uzalishaji mali na biashara badala ya kulitumia kwa kufuata huduma za kijamii pekee.
Kwa upande mwingine Diwani wa Kata ya Marangu Mashariki, Jonas Sombiro Mawala amesema, katika kipindi cha takribani miaka minne kata hiyo imeshuhudia maendeleo makubwa kuliko wakati mwingine wowote ikiwemo upanuzi wa daraja la Marangu Mtoni, ukamilishaji wa daraja la Sembeti - Samanga, ujenzi wa kituo cha afya Marangu Hedikota, ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, matundu ya vyoo, vivuko, miradi ya maji.
Kufuatia taarifa hiyo Dkt Kimei alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujenga, kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali ndani ya jimbo hilo na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo zinazofanywa na Serikali yao.
Dkt Kimei amewataka wananchi wa kata hiyo hususani kijiji cha Sembeti kuwa amepokea uhitaji wa daraja/Kivuko eneo la Kirefure kwenda Marawe Kiura na wanaitafutia utatuzi.
Katika ziara hiyo iliyohusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo pamoja na Mbunge Kimei kukabidhi madawati 50 aliyoichangia shule ya sekondari ya Wasichana Ashira yenye thamani ya shilingi milioni tano.
Walioshiriki ziara hiyo ni kamati ya siasa ya CCM kata ya Marangu Mashariki, wataalam toka ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na MUWSA.
Mwisho..
0 Comments