Na Thobias Mwanakatwe, IRAMBA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba mkoani Singida kimewataka vijana kutumia michezo kujiajiri kwani serikali imeendelea kuboresha mazingira mazuri katika sekta ya michezo .
Katibu wa CCM Wilaya ya Iramba, Mwalimu Ephraim Kolimba,alisema hayo wakati wa ufunguzi wa ligi daraja la nne Wilaya ya Iramba inayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Iramba (IRADIFA) kwa udhamini wa Benki ya NMB tawi la Kiomboi.
Alisema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo hivyo fursa kwa vijana kutumia michezo katika kujiajiri.
Kolimba aliwataka wanamichezo wote wanaoshirikia michuano hiyo kuhakikisha wanacheza kwa nidhamu na uadilifu wa hali ya juu.
"Siku zote nidhamu katika michezo ndiyo silaha ya mafanikio,tujitahidi wanamichezo kuwa na nidhamu ili tuweze kufika mbali zaidi kwani michezo mbali ya kuwa ni burudani kwa sasa ni sehemu ya ajira," alisema Kolimba.
Naye Afisa Mauzo Benki ya NMB Tawi la Kiomboi, Robert Sengo, alisema mbali na kwamba wao kama wadhamini wakuu wa michuano hiyo lakini pia benki hiyo inatoa huduma mbalimbali kwa wateja wao.
Sengo alizitaja huduma zinazotolewa na benki hiyo ambazo wananchi wanatakiwa kuzichangamkoa ni kufungua akaunti ya Chap Chap, huduma za bima pamoja na huduma ya usajili wa kadi za uanachama kwa klabu ya Simba na Yanga kwa gharama ya Sh. 10,000 tu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa MiguuWilaya ya Iramba (IRADIFA),Lucas Mrema almaarufu Kirohosafi alisema kuwa ligi ya mpira wa Miguu daraja la nne Wilaya ya Iramba inayochezwa kwenye kituo cha Ndago uwanja wa Shule ya Msingi Songambele inashirikisha timu nne ambazo zote zitapata nafasi za kushiriki ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa.
Alizitaja timu hizo kuwa ni Kikonge FC,Kibaya FC. Kipuma FC na Songambele FC.
Katika mchezo wa ufunguzi uliofanyika Julai 20,2024 kulikuwa na mchezo kati ya timu ya Kikonge FC na Songambele.
Katika mchezo huo timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 2-2 hali iliyolazimu ziingie kwenye matuta ambapo timu ya Songambele FC iliibuka kidedea baada ya kupata penalti 7 dhidi ya 6 ambazo ilipata timu ya Kikonge FC .
Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Jumapili Julai 28,2024 kwa kuzikutanisha timu za Songambele na Kibaya.
0 Comments