Wanunuzi wa kimataifa 600 kutoka zaidi ya nchi 40 Duniani wanatarijiwa kuhudhuria katika maonyesho ya Karibu-kili fair kwa mwaka 2024 yanayotajiwa kufanyika June 7 hadi 9 katika viwanja vya Magereza mkoani Arusha huku waonyeshaji wakiwa ni 468.
Hayo yalielezwa na mkurugenzi wa maonyesho hayo Dominic Shoo wakati akiongea na waandishi wa habari mkoania Arusha ambapo alisema kuwa Maonyesho hayo yatafunguliwa na waziri wa mali asili na Utalii Angela Kairuki na kwa siku hizo tatu wanatarajia kuwa na biashara kwa kiwango kikubwa kwasababu lengo ni kukutanisha wadau kutoka sehemu mbalimbali Duniani ili kuweza kujua vivutio vilivyopo Tanzania kuvitembelea na kuwa mabalozi wazuri kwaajili ya kuuza vivutio hivyo.
Alisema kuwa mwaka huu onyesho ni kubwa kuliko la mwaka 2023 kwani kumekuwa na ongezeko la waonyeshaji pamoja na kuwa na muamko mkubwa wa wanunuzi kulinganisha na miaka iliyopita ikiwa ni pamoja na kuwa na viwango vya juu zaidi kutokana na vitu walivyoweza kuvinunua ili kuhakikisha maonyesho hayo yanaendana na viwango vya kimataifa.
“Mwaka huu tutakuwa na tamasha la muziki pale pele uwanjani ambao utakuwa ni muziki utakaoleta watu pamoja kwasababu tumeona kwa siku hizi tatu tutakuwa na wageni wengi Arusha ambao hawana burudani ya kutosha kwahiyo kuliko wakapate burudani sehemu tofauti ambazo hazina hadhi tukaamua kuwaandalia kitu kipya ambacho kitawapa burudani June 8 ambapo tumeungana na wataalamu wa burudani,” Alisema Shoo.
Alifafanua kuwa kama wanavyojua biashara ni matangazo na kwa kufanya hivyo wameona utalii unakuwa hasa wakilinganisha na kufunguka kwa msimu wa utalii ambao mwaka huu umefunguka mapema kulinganisha na mwaka jana kwa maana ya kuongezeka kwa kiu ya watu kwenda katika kutembelea mbuga imekuwa ni mkubwa.
“Sababu ya kuongezeka kwa waonyeshaji hii inatokana na watu wana hoteli mpya ambazo ni nyingi, wanabiashara mpya ambazo wanataka kuhakikisha watu wengi wanazijua kwahiyo lengo hasa ni watu wengi kupata taarifa ya biashara hizo na vivutio hivyo ndio maana mwitikio ni mkubwa na wanazidi kuja Tanzania kwani Afrika sisi ndio tunabeba bendera ya utalii,” Alisema.
Aliendelea kusema kuwa ukuaji wa maonyesho hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwatafuta wanunuzi na waonyeshaji ambapo pia wamejipanga ipasavyo katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa hali ya juu kama ilivyo miaka yote na watakuwa na walinzi wasiopungua 300 kwa siku lakini pia wana ulinzi wa Jeshi la polisi.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu kutoka hoteli za Serena Daniel Sambai, alisema kuwa wamekuwa wakionyesha kwenye Karibu kili fair tangu mwanzoni na wameona kila mwaka inaendelea kufanya vizuri na kwa kusema ukweli wamepata wageni wengi na imewasaidia kuongeza biashara yao hapa Tanzania kwahiyo wanafurahi kuwa sehemu ya maonyesho haya tena mwaka huu.
“Tunatarajia maonyesho yatakuwa mazuri zaidi ya yale ya mwaka jana na cha msingi ni kupata wanunuzi ambao wako katika viwango vya juu kwasababu wakiwa wazuri ndio wanaweza kuleta wageni kwetu lakini kwakweli ninawapongeza waandaji kwasababu kila mwaka tunaona ikikua kwa kuleta wanunuzi wenye viwango,” Alieleza Sambai.
0 Comments