Header Ads Widget

GRACE TENDEGA ABADILI UPEPO UBUNGE CCM JIMBO LA KALENGA

 


Na Matukio Daima Media, Iringa

VUGUVUGU la kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu 2025 katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa limeanza kuchukua sura mpya baada ya jina la mwanasiasa maarufu Grace Tendega kuibuka na kuzua mijadala mikali kwenye vijiwe vya siasa, mitandao ya kijamii na hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lenyewe.

Grace Tendega ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Tagamenda, Kata ya Luhota, si mgeni katika medani ya siasa za Tanzania.

 Umaarufu wake unatokana na historia ndefu ya ushiriki wake katika siasa, akiwa miongoni mwa wanawake wachache waliowahi kushika nafasi ya juu ya kisiasa kwa ujasiri mkubwa, siyo tu katika Kalenga bali pia kitaifa.

Kwa mara ya kwanza aliibuka kwenye siasa kupitia chama cha Jahazi Asilia ambapo aligombea ubunge katika Jimbo la Kalenga na kumpa upinzani mkali mgombea wa CCM wa wakati huo, Stephen Galinoma mwaka 2010.

pia Mwaka 2014 katika uchaguzi mdogo wa jimbo la kalenga  kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dkt Wiliam Mgimwa  ,Grace Tendega alijitosa tena kugombea kupitia Chadema na kushika nafasi ya pili huku Geofrey Mgimwa wa CCM akishinda nafasi hiyo .

 Pamoja na kutoshinda, aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kupambana vikali katika ngazi hiyo ndani ya Kalenga, jambo lililomjengea heshima kubwa katika jamii hiyo.


Baadaye alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo aliongeza nguvu ya upinzani katika jimbo hilo.

 Umahiri wake wa kisiasa na uwezo wa kujenga hoja ulimuwezesha kuwa miongoni mwa wawakilishi wa Chadema bungeni kupitia nafasi ya viti maalum, hatua iliyoongeza zaidi ushawishi wake kisiasa.

Hata hivyo, mwaka 2020 alikumbwa na sakata la ndani ya Chadema ambapo yeye na wenzake 18 walifukuzwa uanachama kutokana na msimamo wao wa kuingia bungeni bila ridhaa ya chama. 

Kundi hili maarufu kama "Covid-19" ndani ya Chadema liliwajumuisha pia viongozi waandamizi akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa BAWACHA, Halima Mdee.

Kwa wakati huo, John Mrema akiwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, alithibitisha kuwa baraza kuu la chama kilibariki uamuzi wa kuwavua uanachama na kwamba taarifa hiyo ingewasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa ajili ya hatua zaidi.

 Hata hivyo, Spika wa Bunge, Tulia Ackson, alieleza kwamba suala hilo lilikuwa mikononi mwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokana na taratibu za kikatiba.

Tangu wakati huo, baadhi ya wabunge hao waliotimuliwa wameanza safari mpya za kisiasa kwa kimya kikubwa, huku wakijiunga na vyama vingine. 

Kwa upande wa Grace Tendega, taarifa za ndani sasa zinathibitisha kwamba tayari amejiunga na CCM na anatajwa miongoni mwa wana CCM watakaowania ubunge wa Jimbo la Kalenga kupitia kura za maoni za chama hicho.

Kwa wakazi wa Kalenga, hilo si jambo la kushangaza. Yohana Sanga mkazi wa Ifunda anasema:

"Tangu zamani tumejua huyu mama ni mpambanaji na anaujua mkoa wetu Kama chama kimempokea, sisi kazi yetu ni kutiki tu hatuoni shida na kura za maoni, naamini atakuwa chaguo bora."

 John Ndagula kutoka Tangangozi anaeleza kuwa Kalenga inahitaji mbunge anayejua vipaumbele vyetu kuwa Tendega si mtu wa kuja kujifunza, anavijua vizuri na tunaamini anaweza kutupeleka mbele.

Jina la Grace kuhusishwa tena na siasa za Kalenga limechanganya mahesabu ya baadhi ya wagombea waliotarajiwa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM. 

Awali majina kadhaa yalisikika yakiweka matumaini makubwa, lakini kwa sasa upepo umebadilika.

 Uzoefu wake, historia ya kisiasa na ushawishi wa kitaifa vinampa nafasi ya kipekee katika mbio hizo.

Kwa upande wake, Grace Tendega alipoulizwa na Matukio Daima Media kuhusu nia yake ya kugombea au la, hakuthibitisha moja kwa moja lakini alitoa kauli yenye ishara ya matumaini kwa wafuasi wake.

"Mimi ni mwana Kalenga, muda ukifika nitazungumza Kwa sasa nipo bungeni naendelea kuwatumikia wananchi. Nitarudi kuzungumza nao."

Kauli hiyo imezidi kuleta hamasa kwa wapiga kura wanaosubiri kwa shauku kubwa kusikia msimamo wake rasmi. 

Wengi wanaamini kuwa kauli hiyo ni ishara ya wazi ya nia yake ya kuwania tena ubunge, safari hii kupitia chama tawala.


Jimbo la Kalenga kwa sasa linaongozwa na Mbunge Jackson Kiswaga wa CCM, ambaye alirithi kijiti kutoka kwa  Geofrey Mgimwa. 

Hadi sasa haijajulikana kama Kiswaga atatetea nafasi yake au la, lakini mabadiliko haya mapya ya kisiasa yameleta hekaheka mpya ndani ya CCM Kalenga.

Baadhi ya wana  wa siasa  ndani ya CCM na nje ya CCM wanasema endapo Tendega atatangaza rasmi nia ya kugombea, basi atakuwa mmoja wa wagombea wa kutegemewa kwa makini ndani ya CCM kutokana na historia yake, umaarufu, na uzoefu wake mkubwa.

Tendega  atakuwa na nafasi nzuri ya kuvutia kura za wanawake, vijana na hata watu wa rika la kati wanaotamani mabadiliko yenye uelewa wa siasa na utendaji wa kitaifa.

Kwa sasa macho yote yanakodolewa Kalenga, kusubiri iwapo Grace Tendega atasimama mbele ya umati na kusema yale maneno matatu yenye nguvu kubwa kisiasa: "Natangaza rasmi."


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI