Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp,Dar
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje leo imezindua kampeni maalum ya mgombea nafasi ya Mkurugenzi Mkuu katika Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya kati kwa mbunge Faustine Ndugulile.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo hii Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa kimataifa, Januari Makamba amesema kuwa uchaguzi huo ubahusisha nchi 47 ambapo mpaka sasa nchi 16 zinaiunga mkono Tanzania huku wakiwa wanaendelea na kampeni ya kumtangaza mgombea huyo katika nchi mbalimbali ili waweze kumchagua.
Amesema kuwa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amemteua Mbunge huyo kugombea nafasi hiyo kutokana na uwezo mkubwa alionao wa kuweza kuiwakilisha Tanzania na nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika katika ufanyaji kazi, huku ikiwa nchi 7 zimekubali kuipigia kura Tanzania .
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la kigamboni Faustine Ndugulile ambae ni mgombea wa nafasi hiyo amesema kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo anakwenda kuwakilisha katika kampeni yake ni pamoja na kujenga mifumo imara ikiwa ni pamoja na kuendelea na kampeni ya kuthibiti vifo vya mama na mtoto.
"Namshkuru sana Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua na kupitisha jina langu kuwa mgombea wa nafasi hii, kuna vipaumbele vingi sana ambavyo tunakwenda navyo sisi kama nchi ikiwemo kuboresha mifumo ya teknologia"amesema Mbunge Ndugulile.
Naye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali kupitia wizara hiyo wamepunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80, huku wakiendelea kujipanga kuboresha sekta ya afya na kuleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kusimamia bima ya afya kwa wananchi wote.
"Kupitia mgombea wetu Tanzania itatoa mchango mkubwa katika kutunga sera za afya kwani ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi, licha ya kuisaidia Serikali katika sekta ya afya, lakini pia ameshafanya kazi katika mashirika mbalimbali, mkurugenzi aliemaliza muda wake alikua anatokea Botswana na amehudumu kwa miaka 10, sasa ni zamu ya Tanzania, sifa na uwezo tunao"amesema Waziri Ummy.
0 Comments