Jeshi la Polisi wilayani Igunga mkoani Tabora limewafikisha mahakamani wakulima wawili, Mussa Pasco (39) na Karemela Nkinga (60) wote wakazi wa Kijiji cha Mwasungho Kata ya Nguru kwa tuhuma za kulima bangi.
Wawili hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi wa Wilaya hiyo, Elimajidi Kweyamba aliambia mahakama mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga Lidya Ilunda, kuwa Machi 4, mwaka huu 2024 katika Kijiji cha Mwasungho Kata ya Nguru wilayani hapa, washtakiwa wote wawili walikutwa wamelima bangi miche 26,033 kinyume cha sheria.
Majidi alisema washitakiwa wote wawili walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 11 kifungu kidogo “a” cha sheria ya kuthibiti dawa za kulevya sura na. 95 marejeo ya 2022 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Hata hivyo washitakiwa wote wawili walikana kutenda kosa hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 17, 2024 itakapotajwa ambapo washitakiwa wote wawili wamepelekwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini.
Kila mmoja alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh milioni 8 kila mmoja.
Mwisho.
0 Comments