Header Ads Widget

DCEA YATOA WITO HUU KWA WANANCHI, YASHIRIKI MAONYESHO YA SABASABA

 


Na Fatma Ally Matukio na Habari

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kwa sasa iko katika oparesheni maalum inayoendeshwa katika shule za msingi, Sekondari na vyuo vikuu kwa lengo la kutoa elimu ya kinga kwa vijana ili wafahamu madhara ya utumiaji wa dawa hizo.


Hayo yameelezwa na Kamishna wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, wakati alipotembelea banda la madawa ya kulevya lililopo katika maonyesho ya biashara ya 49 ya kimataifa  yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba.


Amesema kuwa, ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuelimisha jamii kuhusu aina mbalimbali za dawa za kulevya,athari zake kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla, pamoja na hatua kali za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.


Ameongeza kuwa, pia wanaoparesheni ya kuwakamata wale wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya inaendelea kwa nguvu ili kuhakikisha janga hili linatokomezwa kabisa nchini.


"Lengo mahususi la kushiriki kwenye maonyesho haya ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya na sheria zinazohusiana na matumizi, usambazaji na uzalishaji wa dawa hizo haramu"


Ameongeza "tupo hapa ili wananchi wapate elimu ya kutosha kuhusu dawa za kulevya na aina zake,madhara yake,pi wajue kwamba sheria iko wazi kuhusu mtu yeyote atakayekamatwa akiwa anazimiliki, kuzisambaza au kuzitumia" amesema Kamishna Lyimo. 


Akizungumzia hali ya waathirika wa dawa za kulevya,Kamishna Lyimo ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita inatoa huduma za matibabu bila malipo kwa wote walioathirika,ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa.


"Hii ni hatua muhimu ya huruma na uwekezaji wa serikali kwa watu wake. Tunataka kila Mtanzania awe na afya njema na asiwe mateka wa uraibu wa dawa hizi hatari"amesema Kamishna Lyimo.


Pia ameeleza kuwa kutokana na oparesheni mbalimbali zinazoendelea kufanyika nchi nzima, hali ya matumizi na upatikanaji wa dawa za kulevya inazidi kuimarika. Dawa za kulevya hatari kama vile heroin na cocaine zimepungua kwa kiasi kikubwa nchini.


Aidha, DCEA inatoa wito kwa wananchi wote kutembelea banda lao ili kupata elimu ya kina juu ya namna ya kujikinga na madhara ya dawa za kulevya na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya janga hili ambalo lina athiri nguvu ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI