WAJASIRIAMALI Mkoani Pwani wametakiwa kujisajili kisheria na kulipa kodi mbalimbali za serikali ili kuongeza mapato ya serikali ili yaweze kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta wakati akikabidhi vyeti kwa wajasiriamali wenye viwanda vidogo na vidogo kabisa wa mkoa huo ambao wametambuliwa na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Mkoa wa Pwani.
Mchatta amesema kuwa SIDO imefanya kazi kubwa kuwapatia mafunzo na mitaji kwa ajili ya wajasiriamali ambao wameanzisha viwanda vidogo na kuisaidia serikali kuongeza ajira.
Aidha ameipongeza SIDO kwa jitihada za kuwawezesha wajasiriamali ambapo Mkoa huo una jumla ya viwanda 1,533 vikubwa 122 vya kati 120 vidogo 274 na vidogo sana 1,117.
Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Pwani Beata Minga amesema kuwa unatambua jitihada za wajasiriamali ambao wameanzisha viwanda ambavyo vitaongeza ajira na kuongeza pato la mwananchi mkoa na Taifa.
Minga amesema kuwa vyeti hivyo vya kuwatambua vitawasaidia pale wanapohitaji kutambuliwa na taasisi nyingine ambazo ni za uwezeshaji na zoezi hilo litakuwa endelevu ambapo jumla ya wajasiriamali 65 wametambuliwa.
0 Comments