Header Ads Widget

KIWASA,RUWASA WATANGAZA KUMALIZA TATIZO LA MAJI KIBONDO

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MAMLAKA ya maji na usafi wa mazingira  mji wa Kibondo (KIWASA) na Wakala wa maji  na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya  Kibondo zimetangaza mkakati wa kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa wilaya hiyo ifikapo mwaka 2025.


Aidan Ngatomela  Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kibondo

Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji katika mji wa Kibondo (KIWASA), Aidan Ngatomela alisema kuwa mwaka 2021 upatikanaji wa maji katika mji wa Kibondo ulikuwa asilimia 37 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.9 walichopokea kwa miaka mitatu kimewezesha upatikanaji huo wa maji kuongezeka na kufikia asilimia 67.6 iliyopo sasa.

 

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kupitia fedha hizo ipo miradi mbalimbali wanayotekeleza ikiwemo ya kuimarisha vyanzo vya maji, usambazaji wa mtandao wa maji na kwa sasa tatizo kubwa ni matanki ya kuhifadhi maji ambayo yanafanya kiasi kinachozalishwa kusambazwa wakati huo huo kutokana na kutokuwepo kwa matanki ya kuhifadhi kiasi kikubwa cha maji.

 

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa kwa sasa wanakamilisha mradi wa ujenzi wa tanki la kuhifadhi lita milioni 1.5 lenye thamani ya shilingi milioni 400 ambalo ambalo ujenzi umefikia asilimia 75 na kukamilika kwake kutaongeza uhaifadhi wa maji na kufanya kuwepo muda wote hivyo sehemu kubwa ya mji wa Kibondo utakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama.

 

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA wilaya ya Kibondo,Almas Mohamed alisema kuwa walaka huo umepanga kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji vijijini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya uchimbaji visima katika vijiji 12 ambavyo havikuwa na maji kabisa na tayari vijiji sita uchimbaji visima umekamilika.

 

Almas alisema kuwa kwa sasa upatikanaji wa maji vijijini wilaya ya Kibondo umefikia asilimia 75 kutoka asilimia 57 mwaka 2015 na hiyo inatokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo inayogharamiwa na wafadhili na fedha kutoka serikali na mpango ni kuhakikisha huduma ya maji inapatikana ndani ya mita 400 kufikia mwaka 2025.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI