Header Ads Widget

RC MTWARA APONGEZA MKOA WA LINDI KUANZISHA MAONESHO YA MADINI



Na Hadija Omary, Lindi.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, kwa ubunifu wa kuanzisha maonesho ya madini yanayolenga kuonesha utajiri mkubwa uliopo mkoani humo na kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo kuongeza kwa uwezo na kipato.


Kanali Sawala alitoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi mafunzo kwa wachimbaji wadogo yanayofanyika sambamba na maonesho hayo, akisisitiza kuwa elimu wanayoipata itawasaidia kunufaika na rasilimali za madini na kuinua hali zao za kiuchumi.



"Mafunzo haya mtakayoyapata yaende kuwanufaisha ninyi na Watanzania wengine kwa kuwashirikisha elimu wale ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria," alisema Kanali Sawala.


Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Lindi kwa sasa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa madini nchini, hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta hiyo.



"Leo tuko hapa Lindi na tunasema 'Dunia iko hapa, njoo uwekeze'," aliongeza.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo, ambaye ni mwenyeji wa maonesho hayo, alisema Mkoa wa Lindi una maeneo mengi yenye madini, hali inayotoa nafasi kubwa ya kiuchumi kwa wananchi.


Mnufaika wa mafunzo hayo, Mendrad Chikojo, alisema elimu aliyoipata itamuwezesha kuboresha shughuli zake za uchimbaji madini.



"Nilivyofika ni tofauti na nitakavyorudi. Kwa ujumla nimeongeza maarifa na nitaendelea kujivunia maonesho haya kwa kuwa yameniongezea kitu katika shughuli zangu za kila siku," alisema Chikojo.


Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Lindi, Emanuel Shija, alisema mafunzo hayo yanawasaidia wachimbaji wadogo kuelewa sheria, umiliki wa leseni na uwajibikaji katika sekta ya madini.


Aliongeza kuwa taasisi za kifedha zikiwemo benki zimealikwa kutoa elimu kuhusu namna ya kupata mitaji na kuwekeza katika sekta ya madini, jambo linalotarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa madini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI