Header Ads Widget

CHANGAMOTO KUBWA KWA ASKARI POLISI KUSHINDWA KUHIFADHI NA KUSAFIRISHA SAMPULI

 




LICHA ya Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutumia mashine za kisasa ya ofisi ya  za gharama kubwa kupima sampuli kwenye maabara ya mkemia mkuu wa Serikali mbalimbali zikiwemo zinazohusu mashauri ya Jinai Ili haki itendeke, bado baadhi ya maafisa wanaohusika na mnyororo wa haki Jinai wakiwemo askari Polisi wameshindwa kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha sampuli hizo vile inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria 


Hali hiyo imesababisha sampuli zinazokosa ubora kutupwa kwa kushindwa kupimwa hivyo Serikali kuingia gharama ya kurudia upya zoezi hilo ikibidi kulazimika kufukua miili ambayo tayari ilishazikwa Ili kupata sampuli zingine ama kukosa vielelezo vya kufanya Shauri kupata ushahidi wa kutosha usio na shaka mahakamani.


Hayo yameelezwa na Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kanda ya kati, inayohusisha mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Tabora na Morogoro Bw Gerald Meliyo Mollel wakati alipokutana na wadau wa mnyororo wa haki jinai wakiwemo maafisa wa polisi, madaktari, waendesha mashtaka, mahakimu, maafisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na RushwaTAKUKURU/ PCCB kutoka wilaya zote za mkoa wa Morogoro.


Wadau hao  wanakutana mjini Morogoro kujifunza hatua muhimu za ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji salama wa sampuli kwenda maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kwaajili ya kupata vielelezo na ushahidi wa mashauri ya mahakamani.


Meliyo akasema changamoto hizo zimemsukuma Mkemia mkuu wa Serikali kuandaa mafunzo kwa wadau hao katika suala zima la huduma za forensky (Kamisheni ya uchunguzi wa kisayansi) lengo likiwa ni kuwaweka wataalamu hao kwa pamoja kuweza kutatua changamoto zinazotokana na namna ya kujishughulisha na sampuli za kijinai.


“Lengo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhakikisha masuala ya haki jinai na huduma za kiforenskia zinafika katika ngazi za juu ikiwemo mahakama na haki kupatikana kwa watuhumiwa au wanaolalamika, kwa sasa maabara ya mkemia mkuu wa Serikali inafanya uchunguzi wake kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa ambayo ni ya gharama kubwa na Serikali imewekeza nguvu kubwa kabisa katika ofisi yetu ili kuhakikisha haki inatendeka, Rais wetu Mhe Samia Suluhu Hassan ameipa ofisi ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali jicho la kipekee”Alisema Mollel.


Akasema mamlaka hiyo pia ina viwango vya kimataifa vya ISO vnayotambulika duniani kote hivyo sampuli ikichukuliwa hapa na ikapelekwa nchi yeyote duniani matokeo huwa ni sawa.


Kuhusu utupaji wa sampuli akakiri hali hiyo kusababishwa na kupelekwa bila kukidhi matakwa ya kisheria ama kanuni ikiwemo kutojazwa kwa nyaraka mbalimbali za sampuli, kutotosheleza kwa sampuli iliyochukuliwa kwaajili ya vipimo, kutofungashwa vizuri na kuharibika au kuoza hivyo kuwarusisha wahusika.


“Unaporudishwa kuchukua upya sampuli ni gharama, inaongeza gharama kubwa, na ikitokea marehemu tayari ameshazikwa inakuwa ni gharama kufukua upya mwili na kuchukua sampuli nyingine, ndio maana tunahimiza sampuli ichukuliwe kwa usahihi,ifungashwe kwa usahihi, isafirishwe kwa usahihi, kiasi kinachotosheleza, daktari na askari washirikiane kuchukua kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha haki inatendeka”Alisema Meneja huyo.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kamisheni ya uchunguzi wa kisayansi, Forensky, Shaban Hiki, alisema ili vielelezo vya makosa ya jinai vinavyopelekwa ofisi ya Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kwaajili ya uchunguzi wa kimaabara kuweza kutoa matokeo sahihi yatakayotumika kama ushahidi kwenye mashauri ya jinai katika ngazi za mahakama, ni lazima askari na madaktari wanaohusika na uchunguzi kuzingatia usahihi wakati wa uchukuaji, ufungashaji, utunzaji na usafirishaji wa sampuli hizo hadi kwenye maabara kwaajili ya uchunguzi kwa kuzingatia utaalamu na kufuata taratibu zote za kisheria zilizopo.


Akaonya uchukuaji, usafirishaji na utunzaji usio sahihi wa sampuli za uchunguzi wa kimaabara usiozingatia sifa sahihi kwa mujibu wa miongozo na sheria husababisha sampuli hizo kufikishwa kwenye maabara ya mkemia mkuu wa Serikali zikiwa zimeharibika, hazikidhi sifa na sababu zingine zinazofanya kutupwa na hivyo kuchelewesha usikilizwaji wa mashauri ya jinai mahakamani au kufanya mashauri hayo kukosa ushahidi wa kutosha.


“Unaweza kukuta mchukuaji sampuli anachukua kipande kidogo cha ini, ama anakata eneo lisilofaa au anafungasha kwenye vifungashio visivyo sahihi anasababisha zikifikishwa kule zinakuwa zimeharibika, hazifai kwavile ni ndogo na hazitoshelezi na sababu zingine zinazofanya zikifika ziwe rejected (zitupwe), ndio maana tunashauri OCCID (Mkuu wa upelelezi wilaya) wapitishe sampuli hizi kwa barua zije Forenski  ili zikaguliwe kama ziko sahihi kabla ya kupelekwa maabara ya mkemia mkuu wa Serikali”Alisema Kamishna huyo wa Polisi.


Akataka mchakato sahihi kufuatwa ili  kuleta matokeo chanya ya kiuchunguzi na kuwaasa wanaokusanya sampuli au vielelezo wajue aina sahihi ya vifungashio vya sampuli na ujazaji sahihi wa fomu kwa kutumia nakala halisi kwa mujibu wa takwa la sheria ili kukidhi matakwa ya kisheria mahakamani na kukubalika kwa majibu hayo kama kielelezo halali mahakamani kwavile watakuwa na ushahidi usio na shaka.


“Jukumu mojawapo la maabara ya mkemia mkuu wa Serikali ni kufanya uchunguzi wa kimaabara,wa sampuli na vielelezo mbalimbali,na vielelezo vyote vinavyotokana na mashauri ya jinai na kuhitaji matokeo ya uchunguzi wa kimaabara ili kupelekwa mahakamani kama uthibitisho na kutumika kama sehemu ya ushahidi mahakamani, kwahiyo kwa kipekee nimshukuru Mkemia mkuu wa Serikali Dkt Mafumiko na timu yake kwa kuandaa mafunzo haya yatakayoleta tija kwa haki ya jinai na hasa kwa askari wetu wa Jeshi la Polisi, madaktari, mahakimu,waendesha mashtaka,TAKUKURU kwani hawa wote wako kwenye mlolongo wa haki jinai”Alisema Kamishna Hiki. 


Aidha akawataka madaktari kuzingatia usahihi wa ujazaji wa fomu ya polisi namba tatu kwaajili ya matibabu PF3 ili kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa kujazwa ndivyo sivyo.


Naye  Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Joseph Maugo akataja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na kuchelewa kupata majibu ya vipimo vya sampuli kutokana na miongozo, umbali mrefu hasa kwa wanaotoka vijijini kufika Dodoma kupeleka sampuli na kuchelewesha mashauri hasa yasiyo na msukumo mkubwa kisiasa,majibu kutoka tofauti na matarajio, kupokea majadala wakati tayari upelelezi umeanza na sababu zinginezo ingawa akashukuru kwa mafunzo hayo





Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS