Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) umeitaka serikali kutoa majibu kwa vijana ni lini mikopo kwa makundi maalum kupitia halmashauri itarejeshwa ili vijana waweze kunufaika na mikopo hiyo.
Kauli hiyo ya vijana imetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa,Mohamed Kawaida ametoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa Habari mkoani Kigoma akielekeza agizo hilo kwa ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya kazi, ajira vijana na watu wenye ulemavu na wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI.
Akitoa azimio hilo kwa niaba ya wajumbe wa baraza kuu la UVCCM Taifa waliofanya kikao chake cha kawaida mkoani Kigoma Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa amesema kuwa baraza kuu linatoa siku saba kwa wizara hizo mbili kutoa kauli kuhusu jambo hilo na kwamba kushindwa kufanya hivyo kwa siku walizotoa watataka watendaji wa wizara hizo kujitathmini kama wanafaa kuendelea na nafasi zao.
Azimio hilo la baraza kuu la UVCCM linakuja siku mbili baada ya kauli ya Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuharakisha mchakato wa utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum mikopo ambayo ilikuwa imesimamishwa na serikali.
Sambamba na azimio hilo baraza hilo la UVCCM pia limeitaka serikali kushughulikia na kuchukua hatua za haraka kushughulikia tatizo la uhaba wa sukari ili kuwaondolea wananchi ukali wa Maisha wani wamekuwa wakiipata bidhaa hiyo kwa bei kubwa huku kukiwa na mfumuko mkubwa wa bei.
Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM ametangaza azimio la baraza kuu la UVCCM kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji unaoridhisha wa ilani ya uchaguzi ya CCM hasa uboreshaji wa demokrasia nchini kwa kutumia falsafa ya 4R ambao umewaweka Pamoja watu wote nchini.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho cha baraza kuu la UVCCM kiliibuka na azimio la kumpongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM na Raisi wa Zanzibar kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kuimarisha umoja na mshikamano wa watu wote kule Zanzibar.
0 Comments