Header Ads Widget

MADIWANI HALMASHAURI ITIGI WAPITISHA RASIMU MAKISIO BAJETI YA BIL.19.9/- KWA MWAKA 2024/2025

 

Na Thobias Mwanakatwe, ITIGI

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida  limepitisha kwa kauli moja makisio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025  jumla ya Sh.bilioni 19.975 kwa ujetekelezaji wa miradi ya maendeleo, ruzuku ya mishahara na matumizi mengineyo.


Makisio hayo yalipitishwa juzi katika mkutano maalum wa baraza hilo ambao ulikuwa kwa ajili kujadili mapitio ya utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na makadirio ya mipango na bajeti kwa mwaka 2024/2025.

Akiwasilisha rasimu ya makisio ya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Afisa Mipango, Emmanuel Dyelu, alisema fedha hizo Sh.bilioni 13.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh.bilioni 6.4 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.


Dyelu alitoa mchanganuo kuwa katika bajeti hiyo halmashauri imepanga kukusanya Sh.bilioni 2.1 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani,Sh.bilioni 1.6 mapato huru wakati Sh.milioni 426.8 ni mapato lindwa.


Alisema baadhi ya kazi za maendeleo zilizopagwa kutekelezwa na halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari,ukamilishaji wa majengo katika Hospitali ya Wilaya na ujenzi vyumba za watumishi katika shule za msingi,sekondari na vituo kutolea huduma za afya.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa zahanati mpya za Ipangamasasi,ukamilishaji wa nyumba ya watumishi katika kituo cha afya Mitundu,ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari,ujenzi shule mpya ya msingi katika kata ya Bangayega na ujenzi wa sekondari moya kata y Mwamagembe.


Aidha, Dyelu alisema baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mipango ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni ununuzi wa vishikwambi 20 kwa ajili ya uendeshaji wa vikao kidigitali,ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi,usajili wa shule 25 za nsingi na tatu za sekondari na ujenzi wa sekondari mpya ya Majengo.


Mafanikio mengine ni ujenzi wa hosteli moja sekondari ya Mitundu na mabweni mawili katika sekondari za Mgandu na Ipamuda,kujenga vyumba vya madarasa 10 vya sekondari,vyumba tisa vya madarasa katika shule kongwe za msingi na ujenzi wa matundu 270 ya vyoo katika shule za msingi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussein Simba,alisema ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo umekuwa mzuri na kufikia karibu asilimia 82 mapato huru ambayo yakichanganywa na mapato lindwa inakuwa takribani asilimi 70.


Alisema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya madiwani,Mkurugenzi na wataalamu na kwamba ushirikiano huo uzidi kuendelea katika mwaka huu wa fedha ili kiwango cha ukusanyaji mapato kizidi kuongezeka zaidi.


Simba alisema katika bajeti 2024/2025 kumekuwa na ongezeko la asilimia 2 kwenye eneo la zao la pamba na dengu na upande wa biashara kutakuwa na ongezeko ka karibu Sh.bilioni 2 ukilinganisha na bajeti iliyopota ambapo ilikuwa ni Sh.bilioni 2.0.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi,John Mgalula, alisema halmashauri imejipanga kutekeleza miradi yote iliyopanga kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwaletea maendeleo wananchi.


Mgalula alisema changamoto ya ukosefu wa gari la wagonjwa katika kituo cha afya Rungwa, alisema litatatuliwa kwani serikali ilishaahidi kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa ambapo yakiletwa moja kitapelekwa katika kituo hicho cha afya.


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni,Maimuna Likunguni, alisema madiwani na wataalam wasaidie kusimamia suala la ukusanyaji wa mapato kwani kupitisha bajeti ni jambo moja lakini kazi ni kusimamia ukusanyaji mapato.


"Mwaka huu ni uchaguzi wa serikali za mitaa,kufanikiwa kwa bajeti hii itakisaidia chama katika uchaguzi katika kuomba kura kwa wananchi," alisema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI