Na Shamte Nazalary Abas Kiobya
Husemwa kwamba ngamia ilibebeshwa mzigo wa mabua,Kwanza, yaliwekwa mabua kiasi, ikahimili. Mzigo ukaongezwa, ngamia ikaendelea kuhimili. Mzigo ukaogezwa tena, ikaendelea kuhimili. Mzigo ulipoongezwa zaidi, ngamia ilishindwa kuhimili, mgongo wake ukavunjika! Iliaminika kuwa lazima kulikuwepo ubua wa mwisho ambao ulivunja mgongo wa ngamia huyo.
Kinachoendelea nchini mwetu wakati huu, ubinafsishaji wa bandari zetu, kinaweza kufananishwa na kisa hicho cha ngamia na mzigo wa mabua. Sakata la Tanzania kuingia kwenye mkataba na wawekezaji kupitia DPWorld kwa minajili ya kuendesha bandari zote zilizopo nchini, pengine linaweza kuwa bua la mwisho lililovunja mgongo wa ngamia.
Sakata hili limebeba na kufichua mambo mengi ambayo yalikuwa yamejikita kwenye vifua vya idadi tosha ya Watanzania. Mambo ambayo hayakuwa yakizungumzwa waziwazi. DPWorld imekuwa ubua ambao umefunua vifua vya Watanzania hao. Kumbe wananchi hao walihifadhi mengi yenye ukakasi. Wamekuwa wavumilivu, lakini kwa suala hili wameguswa pabaya. Mgongo umeelemewa na kushindwa kuhimili zigo!
Hali ya "na liwalo liwe", imejitokeza. Sakata la DPWorld limefichua hata yale yaliyokuwa upenuni mwa mioyo yao.
Sasa kunasikika Utanganyika na Uzanzibari kutoka pande zote mbili, Visiwani na Bara! Aidha, kutajwa au kudaiwa kwamba kumbe nchini mwetu kuna wenye haki zaidi kuliko wengine. Kama ilivyo kwenye kitabu kiitwacho Shamba la Wanyama (Animal Farm), binadamu wote ni sawa, lakini wengine wana usawa unaozidi wa binadamu wengine (all animals are equal, but some are more equal than others)!
Mathalani, eti nafasi nyeti serikalini zimekuwa za kurithishana. Wengine wamediriki kutaja majina ya viongozi wa ngazi za juu, na msururu wa watoto na ama baba au babu zao na nafasi nyeti nchini wanazohodhi. Wananchi huwa wakijiuliza, hao watoto, wajukuu na vilembwe, wamefikaje hapo walipo! Ni kwa bahati, nyota zao za kipekee au ni kwa kubebana? Je, watoto wengine Wakitanzania hawakusoma vizuri kama hao wenye nyota za kipekee, kwa hiyo kutoweza kushika nyadhifa hizo? Ni dhahiri tabaka la wateule linazidi kushamiri katika ngazi kuu zote za uamuzi nchini. Mifano ni kedekede, ikiwa ni pamoja na bunge, wakuu wa wilaya/mikoa, mahakama, taasisi za kifedha kama Benki kuu na TRA,n.k. Wale ambao hawajawa wateule wakitamani/taka kuwa katika kundi hilo, basi hawana budi kuwa "machawa" wa wateule.
Sio maneno yangu!, wananchi wanaendelea kusema, eti sasa wateule wametokewa kuleta wawekezaji, maana wao ndio wenye nchi. Eti mustakabali wa nchi yetu upo mikononi mwao? Wanafanya watakavyo, hata kufikia kutoa sehemu ya ardhi au mali ya umma kwa wageni, huku wakihalalisha kilichofanyika kwa nguvu zote. Wanashindwa kutambua kwamba unapokula na kipofu, usimshike mkono! Kwa Watanzania, sakata la bandari limeibua kiopofu kuguswa mkono.sina hakika kama ni uhalisia, kwani haya ndio yanasemwa hata wasomi "intellectuals"na wazee wakongwe wa nchi hii wamo, Kulikoni?
Kama Chinua Achebe (mwandishi wa vitabu kutoka Nigeria) aivyosema, Hamkani si shwari tena".( No longer at ease!)
Hata hivyo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuhimiza kuwa, tujisahihishe", basi tuwe na matumaini ya hilo kutekelezwa, hatujachelewa! Nia yawezekana ikawa ni njema lakini mambo hayajakaa sawa ki hivyo! wananchi tuelimishwe bila mbambamba, hakika bado tumevulugwa
shamteabas@gmail.com
0 Comments