Header Ads Widget

JE, MSUKUMO WA VIJANA KATIKA MAANDAMANO YA GEN Z JUNI 2024 UMELETA MABADILIKO GANI KENYA?

Dakika chache baada ya saa nane mchana wa Alhamisi Juni 25, 2024 hali tete iliyokuwa inatokota nje ya majengo ya Bunge la Kenya, iliharibika kabisa na kuwa mbaya. Umati mkubwa wa vijana ambao ulikuwa unakabiliana na polisi wa kuzima ghasia asubuhi hiyo, uliwashinda nguvu maafisa wa usalama na kuvunja ua wa Bunge na hatimaye kuingia ndani.

Ni katika wakati huu ambapo historia ilikuwa inaandikwa na kunakiliwa kwenye vitabu vya kumbukumbu nchini humo. Alipolala muanzilishi wa taifa Mzee Jommo Kenyatta - aliyeshirikiana na MAUMAU kupigania haki za Wakenya – ndipo ambapo vijana walipitia wakielekea ndani ya majengo ya bunge wakitaka kuwashinikiza wabunge kutupilia mbali mswada wa fedha wa 2024 ambo walikuwa wameupitisha.

Risasi zilirindima angani kwa muda ambão kwa waliokuwa wanafuatilia kwenye runinga – ulionekana kama mwaka mzima – na kelele ilipotulia, kilio kilifuata, huku maiti ya vijana kadhaa ikilala nje ya Bunge hilo kwenye barabara ya parliament hapa Nairobi.

Kwa nini Wakenya wanaandamana tena?

Taifa lilijipata katika hali ya wasiwasi mkubwa kufuatia yale yaliyokuwa yametokea mbele ya macho ya taifa na ulimwengu kwa jumla. Baada ya saa kadhaa, Rais William Ruto alilihutubia taifa.

''Yaliyotokea leo, hayakupaswa kufanyika kwa kweli. Taifa limeshuhudia hali mbaya ya usalama ya kuvamiwa kwa Bunge la Kenya, na watu ambao wanapaswa kutambuliwa kama wahalifu wenye njama ya kupendua serikali ya Kenya, na hilo halitakubalika,''alisema Rais Ruto mwendo wa saa moja usiku wa Juni 25.

Matamshi hayo ya kiongozi wa taifa hayakupokelewa vyema na vijana ambao walikuwa wanapigania haki ya uongozi bora na kuitaka serikali ya sasa kuwajibikia udhibiti wa mfumuko wa bei ya bidhaa ambao walihisi ulichangiwa na sera mpya ya serikali ya kuongeza kodi kwa ajili ya kukimu gharama ya matumizi ya serikali.

Wanjiru Wanjira aliyekuwa mstari wa mbele kuwapa motisha vijana kutetea haki zao, alisikitishwa na matamshi haya.

''Katiba ya Kenya inampa raia haki ya kuandamana na kulalamikia anachohisi ni dhuluma dhidi ya haki zake za kibinafsi. Vijana wameuawa, ni kwa nini Rais hazunguia hili na kuwaomba jamaa zao msamaha kwa yaliyowakuta watoto wao.?'

Polisi kutumia nguvu kupita kiasi


Kwa mujibu wa mamalaka ya kuchunguza shughuli za polisi nchini Kenya IPOA kesi mbili za mauaji ya waandamanaji zimefikishwa mahakamani na kwa sasa zinaendelea kusikizwa. Huku wachunguzi wake wakiendelea na kesi nyingine 22 zinazohusisha madai ya polisi kutumia nguvu kupita kisi dhidi ya waandamanaji.

Mamake Rex Masai aliyeuawa katika maandamanos hayo ya Juni 2024, amesisitiza kwamba anataka haki itendeke na kwamba kifo cha mwanawe hakipaswi kupotea hivyo hivyo.

Akijitetea mahakamani mapema wiki jana aliyekuwa kamanda wa operesheni ya polisi kukabiliana na waandamanaji mwaka jana, Doris Muira aliaambia mahakama kwamba polisi hawakufyatulia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.

Mukira aliyesimamia maafisa wa polisi kutoka vituo vitano vya polisi jijini Nairobi kwenye operesheni hiyo alijibu maswali alipohojiwa na kutaja kwamba : ''Ni maafisa ambao wanasimamia ghala la silaha kwenye vituo hivyo vya polisi ambao wanaufahamu wa ni bunduki ngapi na risasi ngapi ambazo zilitolewa kwa polisi waliokuwa kazini wakati huo wa maandamano.''

Hali ya taharuki iliposhuka barabarani, mambo yalizidi kuchemka katika uongozi wa polisi, na mojawapo wa wale walioangukiwa na shoka ni aliyekuwa Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome aliyejiondoa kazini kutokana na lalama za vijana na Wabunge na Mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Zaidi ya watu 100,000 waliingia katika mitaa ya mji mkuu, Nairobi, tarehe 25 Juni 2024 kuwashinikiza Wabunge kutopitisha mswada tata wa fedha.

Douglas Kanja alimrithi wa Japhet Koome na kuanza kazi mara moja, ila masuala ambayo vijana walilalmikia mwanzoni bado yaliendelea kushuhudiwa nchini.

Sauti zao kukosoa serikali barabarani walizipeleka mitandaoni, na kuendeleza maandamanos hayo huko. Ila hilo halikupokelewa vyema na serikali.

Waziri Kiongozi Musalia Mudavadi aliwaonya vijana dhidi ya kutowaheshimu wakuu wao.

''Ni muhimu kutofanya mambo mengine ambayo sio tabia njema. Kuweka picha ya kiongozi kwenye jeneza sio jambo zuri kabisa. Vijana tafadhalini muache hayo. Kuna njia mbalimbali za kueleza malalmishi yenu.'' Alisema katika halfa ya mazishi katika huko Vihiga, magharibi mwa Kenya.

Ila visa vya vijana kutoweka na kupatikana wakiwa hali mbaya vimeendelea kushuhudiwa nchini katika mwaka mmoja uliopita. Vijana kama Kibet Bull aliyechora katuni ya Rais Ruto akiwa amelala kwenye jeneza alitekwa na kuachiliwa huru baada ya wiki chache akiwa hajielewi.

Rais William Ruto ametoa taarifa za kukinzana kuhusu utekaji nyara nchini, mwanzo alisisitiza kwamba sio polisi wanaowateka nyara vijana kwa ajili ya kuwatesa. Lakini miezi michache baadaye, akiwajibu wakosoaji kutoka mataifa ya magharibi Rais alisema kwamba,

''Wale wote waliokuwa wamepotea wamepatikana na kurejea nyumbani kwa famiia zao.''

Mwnaharakati Wanjira anatatizwa na hali ilivyo hasa kutokana na uhuru wa kujieleza unavyo kiukwa.

''Sijui ni kwa nini katiba haifuatwi. Hadi wa leo kuna vijana ambão bado hawajulikani walipo. Tulimuona Mbunge mmoja akidai kwamba vijana ndio wanaopanga na kujiteka nyara kwa ajili ya kupokea fidia au kupata umaarufu mitandaoni.'' Alisema Wanjira.

Kimani Uchungw'a ambaye ni Kiongozi wa Wengi Bungeni, alilazimika kuomba msamaha kufuatia tamko hilo lililowakera wengi hasa wazazi wa vijana ambao walipotea na miili yao kupatikana baada ya muda.

Uwajibikaji wa polisi upo?


Mtaalamu wa masuala ya usalama George Musamali anasisitiza kwamba ukosefu wa uhuru wa polisi ndio chanzo cha matatizo haya yote. Na japo rais amesisitiza kwamba ameipa huduma ya polisi uhuru wa kazi kwa kumpa Inspekta Mkuu uhuru wa kifedha na kuweza kufadhili bajeti ya polisi ipasavyo, polisi hawaonekani kuwa huru.

''Tangu Juni 25 2024, maandamano kadhaa yameandaliwa nchini ikiwemo yale ya kukashifu mauaji ya Albert Ojwang aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi. Watu walipigwa risasi na polisi na kujeruhiwa vibaya. Kuna haja ya kila afisa wa polisi kuwajibika akiwa kazini.'

Musamali anasema kwamba makamanda wanaofanya mipango ya kudhibiti usalama kwenye maandamano wanapaswa kufahamu kanuni za polisi kuhusiana na udhibiti wa ummati wa watu na matumizi ya silaha za polisi katika hali ngumu.

''Wiki iliyopita tumeshuhudia maandamano na polisi tena wametumia nguvu kupita kiasi, na sasa kuna wawili kati yao wanakabiliwa na mashtaka ya jaribio la mauaj mahakamani. Polisi wanapaswa kutoegemea upande wowote wa kisiasa na tulivyoshuhudia ni kama wao pia wanaogopa adhabu kali kiwa tatizo litatokea kwenye maandamano hayo,''alisema Musamali.

Viongozi wa kisiasa wamelaumiwa kuingilia kati na kuwatuma vijana kuvuruga maandamano hayo na kutatiza hali ya usalama wa mji wa Nairobi.

Jim India anasema kwa mtazamo wake, vijana wanapaswa kuendelea kuishinikiza serikali ili kuhakikisha kwamba sauti yao imesikika.

''Serikali inaelewa lugha moja, maandamano, na kila tunapoandamana na kusimama tunawapa nguvu ya kujipanga kutudhibiti na kutunyamazisha, manake yale yote tuliyokuwa tunayalalamikia wakati huo, hayajatimizwa na mambo ni magumu hasa kwa mshahara mdogo ambao wenye ajira wanapokea. Gharama ya kodi iko juu sana. Itabidi tuendeleze msukumo huo.''

Barack Muluka ambyae ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi anasema kwamba tangu hapo mambo yamekuwa magumu kwa vijana na msukumo wao kuwawajibisha walio uongozini.

''Rose Njeri aliyebuni mtandao wa kutoa maoni kuhusu mswada wa fedha wa 2025 na kustakiwa kwa matumizi mabaya ya kompyuta lakini aliondolewa mashtaka hayo baada ya ushahidi kukosekana.

Albert Ojwang ameuawa, kuna mama aliyepoteza mtoto akiwa amezuiliwa polisi, na kuna wengine wengi ambao hali yao haijajulikana hadharani, Rais anaonekana kufumbia macho haya na kuendelea kufanya kazi ni kana kwamba haelewi kinachoendelea,''


Je suala la ugumu wa maisha kwa vijana na ukosefu wa ajira limetatuliwa?


Vijana wasio na ajira wanasema kodi zaidi ni mbaya kwa uchumi unaosuasua

Jim India ambaye alikuwa mstari wa mbele wakati huo, aliiambia BBC katika mahojiano wakati huo kwamba: ''Hali ya maisha imekuwa ngumu hadi hatuna chochote mfukoni. Na kama vijana hata pendekezo la sisi kujituma kikazi na kibishara ni jambo gumu kuteeleza ikiwa hauna hata mtaji wa kuanzisha biashara.''

Mwaka mmoja baadaye, vijana bado wanalalamikia ukosefu wa ajira, huku baadhi wakionekana kupoteza matumaini maishani.

Serikali kwa upande wake imesema kwamba imetoa fursa kwa vijana kama vile Mpango wa ufadhili wa biashara kupitia mkopo wa HUSTLER FUND ambao aliuzindua Rais William Ruto punde tu alipochukuwa madaraka mnamo 2022.

Akihutubia kikao cha vijana jijini Nairobi Mwezi Desemba 2024, rais Ruto aliwataka vijana wanaopokea mkopo huo kulipa ili wenzao pia wafaidike na Mpango huo.

Wakati huo, serikali ilikuwa inarekodi kwamba takriban watu milioni nne waliopokea mkopo wa hustler fund hawakuwa wamelipa, hali ambayo inatatiza mpango wa serikali kutoa nafasi kwa vijana kujitegemea.

''Ikiwa watu hawa watalipa madeni yao, kuna fursa kubwa kwao kupata mikopo mikubwa zaidi na kuwawezesha kupanua biashara zao na hali hiyo pia itachangia ukuwaji wa uchumi wa Kenya.''

Lakini kwa vijana kama Bevalyne Kwamboka, serikali haikuchukuwa muda kuwasikiliza malililo yao wakati huo na hata sasa. Kama mfanyabiashara na mwanaharakati wa kutete haki za vijana, Bevalyne amesema kwamba biashara yake ya kupika vibanzi mjini Najirobi ilikwama kutokana na yeye kutoweza kukimu gharama ya maisha.

''Bei ya bidhaa muhimu imepanda na imenibidi nirudi vijijini kupanga upya jinsi nitakavyo anza tena maisha. Japo nimesoma na kufuzu chuoni na shahada, sijapata kazi na sijaridhishwa na jinsi mamlaka inavyojaribu kuzima sauti zetu.' Alisema Kwamboka.

Uchumi umeathirika vipi baada ya maandamano ya Juni 25 2024?

Julians Amboko ambaye ni mtaalamu wa {public finance} na mwanahabari anasema kwamba kutokana na maandamanos haya Rais alipoamua kuidhinisha mswada huo kuwa sheria, serikali imelazimika kuweka mikakati ya kujisitiri ili kutoshindwa kuendesha mambo ya usimamizi wa kitaifa.

'Kutokana na hali hiyo kumekuwa na changamoto kubwa ya serikali kukusanya ushuru. Katiak mwaka huo wa kifedha serikali imekusanya shilingi bilioni 253 ingawa ilikuw aimepangia kukusanya trilioni 2.255 sawia na dola bilioni 17.5 za Marekani. ' alisema Amboko.

Kwa kuwa mswada wa fedha wa 2024 ulianguka serikali imejaribu iwezavyo kufanya uhamasishaji katika jamii na kuwasiliana na wananchi ikiazimia kuwashawishi kuhsiriki katika kuboresha sera zake.

'Mswada wa fedha wa 2025 umewasilishwa kwa raia na wamepata fursa ya kutoa maoni katika kiwango cha kila kaunti ambapo raia walihusishwa,' alisema amboko akiongezea kwamba, ''Changamoto iliopo kwa sasa ni kwamba kuondolewa kwa mswada wa 2024 wa fedha na ukosefu wa Mamalaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA) kutofikia kiwango cha kodi iliyokadiria kukusanyakuna maanisha kwamba matarajio ya shirika la fedha la kimataifa IMF hayatatimizwa.

Mpango wa IMF na Kenya uliotarajiwa kugharamia takriban dola bilioni 3.6 za Kimarekani ukifutiliwa mbali miezi michache kabla ya kuanzishwa rasmi. Hii ilikuwa hatua kubwa iliyoathiri Kenya kutokana na taifa hilo kutotimiza matakwa ya kifedha ya IMF.' Alisema Amboko.

Mbali na uchumi, uismamizi wa nchi umebadilika katika mwaka huu?

Wiki chache baada ya matukio ya Juni 25, Rais Willia Ruto alivunjilia mbali baraza lake la mawaziri na kuteuwa mawaziri wapya ambao baadhi yao walitokea chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM anachokiongoza Raila Odinga.

Waliokuwa manaibu wake chamani Hassan Ali Joho na Wycliffe Oparanya walijiondoa kwenye nyadhifa zao pindi tu Rais Ruto alipowateuwa kama Mawaziri katika serikali Iinayowajumuisha washika dau wote, ambayo kwa sasa inatambuliwa kama BROAD BASED.

Barack Muluka – mchambuzi wa siasa na uongozi – anasema kwamba hatua hii ya Ruto kumleta karibu Odinga ni mbinu ya kumtuliza na kunyamazisha kisiasa.

''Raila alikuwa kidonda ndugu kwa serikali ya sasa na kumuweka karibu ni mbinu ya kuitatiza upinzani.'' alisema.

Hata hivyo Raila mwenyewe amesisitiza kwamba makubaliaono kati ya chama chake cha ODM na kile cha Rais Ruto cha UDA ni ya kimkakati na yanaongozwa na masuala 10 muhimu ambayo wanayakata serikali kuangazia ikiwemo uhuru wa kujieleza, hali ngumu ya maisha miongoni mwa mengine mengi.

''Tumeona katika mwaka huu, mabadiliko katika ofisi ya pili kuu nchini, Rigathi Gachagua aliondolewa mamlakani na nafasi yake kuchukuliwa na Kithure Kindiki. Katika muda huu ambapo amekuwa nje, Rigathi amekuwa mpinzani mkubwa wa Ruto na hata amewazungumzia vijana kupitia mitandao ya kijami kujaribu kuwashawishi kwamba anafaa, ila hilo halitafanikiwa kwa ukubwa kwa sababu ameegemea kupata uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya na sio sehemu nyingine nchini,' alisema Muluka.

Kuhusu suala la ikiwa vijana wamepata haki waliokuwa wakiisaka katika maandamano ya 2024? Muluka anasema kwamba hilo halijafanyika.

''Mabadiliko machache aliyoyafanya Rais serikalini ilikuwa tu kama kuwafumba macho wengi, ilikuwa ni mpangilio tu wa kisiasa,' 'alisema Muluka.

Maoni yake yameungwa mkono na Jim India ambaye anahisi kwamba Rais alikabiliana na suala la maandamano ya vijana kisiasa na hayi sio masuala yanayogusa maisha ya Mkenya wa kawaida.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ameteta msimamo wa serikali mara kadhaa akilitaka taifa kuipa serikali ya sasa nafasi ya kuwahudumia wananchi ipasavyo.

''Serikali imeangazia suala la makazi ya watu kupitia mradi wa nyumba za bei nafuu, vile vile kunasuala la bima ya afya ya SHA ya kuhakikisha kwamba kila mkenya anapokea matibabu inavyopaswa bila ya kubaguliwa na kwa sasa tunaangazia mipangilio ya kuboresha mfumo wa elimu ya msingi nchini,' Mwaura aliwaambia wanahabari katika kikao chake cha kila wiki na wanahabari.

Je, haki za kibinadamu zinaheshimiwa?

Mwaharakati na Afisa Mkuu wa Shirika la Vocal Afrika Hussein Khalid anahisi kwamba juhudi za vijana za mwaka jana zimabadili mambo na mtazamo wa hata vizazi vingine nchini.

''Kama mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu, vuguvugu la kutetea haki za binadamu limepiga hatua kubwa ikizingatiwa mafanikio madogo katika muongo mmoja uliopita. Maandamano haya yamebadili mtazamo wa wengi nchini na Wekenya wengi wanaelewa umuhimu wa kutetea haki zao na kutonyamaza kwani mabadiliko hayapatikani kwa kukaa kimya,'' alisema Khalid.

Khalid aidha anasema japo kuna changamoto ambazo bado zinajitokeza, walio katika nyadhifa za uongozi wameonyeshwa kwamba ukiukaji wa haki hasa katika maanadamano na mauaji ya watu yanakumbana na mapokezi makali kutoka kwa Wakenya.

''Ni wakati wa raia sasa kuwajibika na kuwakosoa viongozi na kuwahitaji kujukumikia majukumu ambayo raia waliwapokeza huku raia nao wakitakiwa kuangazia kwa kina yote ambayo yanatekelezwa na uongozi kwa ajili ya kupata haki,' alisema Khalid.

Lakini kwa vijana Jim India, Kwamboka na Wanjira, bado kuna masuala ya kujionyesha kuishi maisha ya hali ya juu miongoni mwa viongozi wakati ambapo kuna baadhi ambao hawajui riziki itatoka wapi, hilo bado ni jambo ambalo linawauma.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI