Na Nazalary Abas Kiobya shamteabas@gmail.com
Mwezi huu wa Desemba, 2023 Waziri wa TAMISEMI, Ofisi ya Rais, Mh. Mchengerwa* akiwa ameandamana na viongozi waandamizi katika wizara hiyo walifika mjini Bukoba kwa minajili ya uzinduzi wa Miradi ya Maendeleo Mijini (TACTIC).
Tulishuhudia utiaji wa saini kuhusu ujenzi wa soko jipya mjini Bukoba, ujenzi wa stendi ya kisasa ya Kyakailabwa (kwenye kiunga cha mji wa Bukoba), ujenzi wa kingo za mto Kanoni (mjini Bukoba) na ujenzi wa barabara za lami mjini Bukoba zenye urefu wa kilomita saba (7) zitakazowekewa taa pembezoni. Siku hiyo hata mji wenyewe ulizinduka, kama vile ulikuwa umetelekezwa!
Hakika, kwa wana-Kagera tukio hilo limeleta si tu faraja, bali pia furaha isiyo na kifani. Hatimaye kilio kilichokejeliwa cha mbunge wa jimbo la Bukoba mjini, *Mh. Stephen Byabato,* kwenye mkutano uliofanyika katika stendi ya zamani ya mabasi siku ya uzinduzi wa kujenga upya stendi hiyo, kimezaa matunda. Isitoshe, matokeo ya kilio hicho yamewaduwaza wale waliombeza wakiamini kwamba alikuwa akifanya usanii! Mbunge amefutwa machozi na Rais Samia kwa kuyapa kipaumbele maombi yake. Si siri ya kuwa kiasi maridhawa cha fedha kimetolewa kuwezesha utekelezaji wa miradi tajwa.
Bila ya shaka, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, mama mpambanaji, Fatuma Mwasa, atasimamia miradi hii ipasavyo kwa kuzingatia thamani ya fedha na viwango kubalika.
Aidha, Waziri Mchengerwa alitoa angalizo kwa wale watakaodiriki kuingilia miradi hii kwa lengo la kuikwamisha! Alionya wale waliozoea kufanya hivyo huko nyuma, wawe viongozi wa kisiasa au madiwani, zamu hii wakijaribu watakiona cha mtemakuni. Mathalan, hatasita kuvunja baraza la madiwani, kwani ni saizi yake kwa mamlaka aliyo nayo.
Wana-Kagera, kwa mwaka tunaotarajia wa 2024, nasi tuwe wapya. Ujio wa Mh. Mchengerwa umekuwa chachu na ari katika kufufuka kwa matumaini ya kuwepo fanaka mkoani Kagera. Tukubaliane na somo lake alilolitoa kwa kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa manufaa yetu maana tumechelewa mno, tumedumaa. Tusiwe kama Yohana mjinga kwenye kisa katika kitabu cha "Someni bila shida". Yohana alitumwa dukani kununua maziwa. Sarafu aliyopewa kuitumia kununua maziwa aliishika mkononi. Akiwa njiani, alirusha sarafu hiyo na kuipoteza alipotaka kupopoa ndege. Hivyo, alirudi nyumbani mikono mitupu! Alikanywa na kupewa funzo kwamba siku nyingine akitumwa, basi hicho kitu alichotumwa akiweke mfukoni. Wakati fulani alitumwa dukani kununua maziwa. Kwa vile hakuwa makini bali mtu wa kukariri tu, baada ya kununua maziwa, aliyamimina kwenye mfuko wa kaptura, yote yakachuruzika!
Sasa tumepewa fursa nyingine adimu ya kutuletea maendeleo na kutoka kwenye udumavu. Tuachane na ujuaji, ubinafsi na mabishano yasiyo na tija tusije tukapoteza miradi hii kama ambavyo imewahi kutokea huko nyuma. Miaka iliyopita, kuna miradi ambayo ilihamishiwa mikoa mingine baada ya kujitokeza mkoani mwetu malumbano ambayo hayakuwa ya lazima. Tupige moyo konde na kujirudi, tusije tukaenda kapa kama Yohana mjinga alivyorejea nyumbani akiwa mikono mitupu.
0 Comments