Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Vijana 27,000 kutoka kata 17 za wilaya tano mkoani Kigoma wamepatiwa elimu ya afya ya uzazi na stadi za Maisha ikiwa ni mpango wa kuwalinda vijana hao na mimba za utotoni.
Mkunga Mshauri kutoka Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA),Lucy Mabada alisema hayo kwenye tamasha la kupinga ukatili lililofanyika kwenye Kijiji cha Murufiti wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea kilele cha siku ya kupinga ukatili duniani.
Mabada alisema kuwa idadi hiyo inaanzia mwaka 2018 TAMA walipoanzisha mradi huo wa elimu kwa vijana ambapo mradi umegundua kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wasichana wadogo ni kutokuwa na elimu na taarifa kuhusu masuala ya afya ya uzazi hivyo kujiiingiza kwenye suala la mapenzi bila kujua athari za matendo hayo.
Kutokana na hali hiyo alisema kuwa mradi unaojulikana kama ujana wangu nguvu yangu umeweza kufundisha waelimishaji rika katika jamii 55, kuunda makundi 18 katika kata 17 ambapo vijana 270 wameunda makundi ili kupeana maarifa na kuanzisha miradi ya Pamoja.
Akizungumza katika tamasha hilo Diwani wa kata ya Murufiti, Evarist Madandi alisema kuwa mimba kwa wasichana wadogo nchini bado tatizo kubwa ambapo kwa sasa ni asilimia 15 ya wasichana wadogo ndiyo wenye uelewa wa masuala ya afya ya uzazi na athari za mimba kwenye umri mdogo.
Kwa upande wake Afisa Tabibu katika zahanati ya Murufiti, Fabiano Madebo alisema kuwa uzazi pingamizi ni changamoto kubwa inayowakuta wasichana wanaoifungua kwenye umri mdogo na kwamba pamoja na juhudi za watoa huduma za afya kwenye vituo mbalimbali kutumia utaalam wao bado wengi wa wasichana hao wamekabiliwa na matatizo mbalimbali , vilema na wengine kupoteza maisha.
Mwisho.
0 Comments