Katibu wa kanisa la RC Jimbo la Njombe Padre Athanas Mgimba
Na Gabriel Kilamlya, Matukio DaimaAPP NJOMBE
VIONGOZI wa dini mkoani Njombe wametakiwa kutumia nyumba za ibada kuhubiri amani ili kusaidia kukomesha matukio ya mauaji,ujambazi,ubakaji na ulawiti ambayo yameripotiwa kutokea mara kwa mara katika jamii mkoani hapa.
MKuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa, alisema hayo wakati wa tamasha la Upendo lililoandaliwa na Kanisa Katoliki jimbo la Njombe kupitia kwaya ya Mtakatifu Mbaga Tuzinde.
Katika tamasha hilo ambalo lilikuwa ni kwa ajili ya kuchangisha fedha za bima ya afya kwa watoto yatima na walemavu 600 wa kituo cha Inuka Wanging'ombe, Kasongwa alimwakilisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange.
Kasongwa alisema matukio yanayoendelea mkoani Njombe yanatisha na hayaleti afya kwa jamii kwani mbali na ukatili huo pia ripoti iliyotolewa na rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita imebainisha Mkoa wa Njombe una ongezeko kubwa la mimba za utotoni ambao ni ukatili pia.
Naye Katibu wa Kanisa hilo, Padre Athanas Mgimba alisema kituo cha Inuka kilianzishwa kutokana na ongezeko la watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo wanaotokana na wazazi wao kukumbwa na ukatili pamoja na kutelekezwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Walezi wa kwaya ya Mtakatifu Mbaga Tuzinde, Deogratias Mtewele alisema kupitia uinjilishaji waumini wanapata elimu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili pamoja na mahubiri mbalimbali.
0 Comments