Na Willium Paul, Moshi
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro umelaani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambavyo vimekithiri katika kata ya Mwika Kusini.
Kutokana na hali hiyo, UWT imewataka wanawake kuwafichua wanaofanya vitendo hivyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kilimanjaro, Elizabeth Minde, alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya juma la wanawake Wilaya ya Moshi vijijini yaliyofanyika katika kata ya Makuyuni.
Maadhimisho hayo yalienda sanjari na kutembelea wagonjwa na kuwafariji katika hospitali ya Faraja pamoja na kituo cha Afya cha Himo.
Minde alisema kata ya Mwika Kusini inaongoza kuwa na matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto na Wanawake.
“Matukio ya ukatili na unyanyasaji wa watoto na wanawake kata ya Mwika yamekuwa kama mambo ya kawaida kabisa, UWT Mkoa wa Kilimanjaro tunasema sasa basi tuwaombe wakinamama tuunganisheni nguvu zetu kupinga vitendo hivyo kwa kuwafichua waharifu," alisema.
Aidha, Mwenyekiti huyo alifika katika kituo cha afya cha Himo na kushuhudia changamoto zinazokikabili ikiwemo uhaba wa jengo la kulaza wagonjwa huku pia kukiwa na kitanda kimoja cha kujifungulia wakinamama wajawazito hali inayosababisha wajawazito kujifungua kwa zamu.
“Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikipambana katika kuboresha sekta ya afya japo bado zipo changamoto lakini niwahakikishie serikali yenu ni sikivu itatatua matatizo yote kwa awamu hivyo niwasihi watumishi wa afya msikate tamaa endeleeni kuwahudumia wananchi," alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Himo, Dkt. Sudi Muhamed alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) na kwamba tatizo hilo ni kubwa kwani wakinamama wajawazito wanaposhindwa kujifungua kwa njia ya kawaida wanalazmika kupewa barua ya rufaa kwenda hospitali kubwa ambapo inakuwa changamoto kupata usafiri.
Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa jengo la kulaza wagonjwa hali inayowalazimu kugeuza jengo la utawala kuwa wodi ya kulaza wagonjwa ambalo hata hivyo ni finyu .
“Kituo hiki wakati kinaanzishwa kilikuwa kindelezwe ili kupewa hadhi ya kituo cha afya kuwe na jengo la kuhifadhia maiti, na pia kuwe na jengo la baba, mama na mtoto wala hakuna jengo la upasuaji wa dharura kwa wakinamama wajawazito walioshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida” alisema.
Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi vijijini, Ruaichi Kaale alisema kuwa katika wiki ya maadhimisho ya UWT wameamua kutumia siku hiyo kutembelea wagonjwa na kuwafariji kwa kuwapa vitu ili na wao wajisikia kama chama na Serikali kinawajali.
0 Comments