Na Willium Paul, SAME
MASHINDANO ya mpira wa miguu yajulikanayo kama ‘Samia Cup’ katik jimbo la Same Mashariki wilayani Same mkoa Kilimanjaro yataanza kutimua vumbi Novemba 1 mwaka huu.
Mashindano hayo ambayo yameandaliwa na Mbunge wa Same Mashariki,Anne Kilango Malechela, yatazishirikisha timu 91 kutoka kata 14 za jimbo hilo ambapo yatakuwa yakifanyika katika viwanja 32 tofauti.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Semu Mmamba alisema kuwa mpaka sasa maandalizi yameshakamilika ambapo yatazinduliwa na katika kata ya Mpinji tarafa ya Mamba vunta.
Mmamba alisema kuwa, mashindano hayo yanafadhiliwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambapo mgeni rasmi atakuwa Katibu Uhamasishaji na Chipukizi Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Edna Lameck.
Alisema lengo la mbunge kuanzisha mashindano hayo ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani za kuinua vijana kupitia michezo pamoja na kutangaza kazi mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
“Hadi sasa maandalizi yameshakamilika ambapo viwanja vyote vipo katika hali nzuri hivyo niwaombe wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji mbalimbali vinavyopatikana katika jimbo la Same mashariki na ligi hii inatarajia kufika kilele chake mwezi Februari mwaka,” alisema Mmamba.
0 Comments