Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza kusambaza vyandarua 341,000 kwa shule za msingi zilizopo katika halmashauri sita za mkoa wa Singida lengo ikiwa ni kuhakikisha malengo ya taifa ya kutokomeza malaria ifikapo 2030 yanatimia.
Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, akizungumza jana wakati uzinduzi na uhamasishaji wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua kwa shule za msingi za Mkoa wa Singida, alisema zoezi hilo litachukua wiki tatu kukamilika.
Alisema MSD imepewa jukumu la kusambaza vyandarua hivyo kutokana na uzoefu wa kusambaza dawa na vifaa tiba nchini na uwepo wa miundombinu ya usafiri na miundombinu ya kielektroniki.
"Matarajio ya MSD ni kwamba kwasababu lengo la nchi ni kuwa ifikapo 2030 ni kuondoa malaria, hivyo MSD inapita katika lengo hilo hilo la taifa na kwa mkoa wa Singida halmashauri zitakazogawiwa vyadarua hivyo ni Iramba,Mkalama,Singida DC, Ikungi,Manyoni na Itigi," alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba, alisema serikali zote kuanzia awamu ya kwanza hadi ya sita imekuwa ba malengo ya kupambana na Malaria kwa kuwakinga wananchi dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwagawia vyandarua vyenye dawa bila malipo.
Alisema ugonjwa wa malaria bado ni tatizo katika mkoa wa Singida kutokana na utafiti uliofanyika 2022 ukionesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kuwa ni asilimia 1.5.
Serukamba alisema kutokana kiwango hicho cha maambuzi serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na ugawaji wa vyandarua ,kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Njia nyingine zinazotumika katika kuhakikisha serikali inatokomeza kabisa malaria ifikapo 2030 ni kuimarisha ufuatiliaji na tathimini ya mipango ya Malaria kitaifa unalenga kuwa na maambukizi chini ya asilimia 3.5 ifikapo 2025 na kuhamasisha jamii juu ya afua mbalimbaliza udhibiti wa malaria.
Serukamba aliziagiza halmashauri kutenga fedha katika mapato yao kwa ajili ya kununulia dawa za kuulia mazalia ya Mbu na kuagiza kila mwanafunzi atakayepewa chandarua kitumike kwa matumizi sahihi ili kuendeleza mapambano dhidi ya Malaria.
Naye Mwakilishi wa Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, Theresia Shirima, alisema wananchi wahakikikishe wanavitumia vyandarua hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na halmashauri zitunge sheria ndogo kudhibiti watakaovitumia kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.
"Vyandarua hivi kimsingi sio vya bure vimewafikia wananchi kwa bure tu lakini ukwelu serikali imetumia gharama nyingi kuvinunua hadi kuvifikisha kwa jamii," alisema.
Shirima alisema mikoa ya Tabora,Mtwara,Kagera na mikoa ya kusini kiwango cha maambukizi ya Malaria kipo juu.
MWISHO
0 Comments