Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amezindua Mradi wa Kijani Hai ambao unalenga kilimo kinachozalisha kisichoharibu mazingira ambao utawanufaisha zaidi ya wakulima 300,000 huku akiwataka wakulima kuzingatia kilimo hai kwa kuwa mazao yanayozalishwa kupitia kilimo hicho yana soko kubwa katika masoko ya kimataifa.
Akizungumza leo (Oktoba 24, 2023) na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maafisa kilimo na wakulima kutoka mikoa ya Singida na Simiyu ambako mradi huo utaendeshwa katika mafunzo yanayofanyika mjini Singida, alisema ni ukweli usiopingika kuwa mazao yanayolimwa kwa kilimo hai yana soko kubwa na yanaweza kuuzwa katika soko lolote duniani.
"Dunia ya sasa lazima uanzie sokoni, ulime kitu ambacho kina mnunuzi si wakati wa kulima tu hujui nani atanunua,tulime tukijua mnunuzi ni nani na tukilima tukijua mnunuzi ni nani tutalima kulingana na masharti yake",alisema.
Serukamba alisema hivi sasa kuna tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira hivyo ifike wakati shughuli za uzalishaji ziendane na kuokoa mazingira kwa kuendesha kilimo ambacho hakiharibu ardhi.
"Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisitiza kutunza mazingira kwenye kilimo na vyanzo vya maji hivyo naziagiza halmashauri kuwaelimisha wakulima kutumia kilimo hai ambacho hakiharibu mazingira na pia soko la mazao yanayozalisha kwa njia ya kilimo hicho yana soko," alisema.
Aidha, alisisitiza suala la matumizi ya mbolea ya asili ili kupata mazao hai na kulinda ardhi iendelee kuwa hai na kwamba mikoa ya Singida na Simiyu itaendelea kutoa ushirikiano katika kilimo hai ili wakulima wajikite kwenye kilimo hicho.
Naye Kiongozi wa Mradi wa Kijani Hai,Andrew Mphuru, alisema mradi huu ambao utaendeshwa kwa miaka mitano kuanzia 2023 hadi 2028 utawanufaisha wakulima 300,000 wa mikoa ya Singida na Simiyu na utagharimu zaidi ya Sh.bilioni 4.
Alisema mradi huu ambao utaendeshwa na Shirika la Helvetas kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ)/kwa ufadhili wa Laudes Foundation la Uholanzi wakulima watapewa mafunzo ya namna ya kuendesha kilimo hai cha pamba.
Mphuru alisema lengo la mradi huu ni uzalishaji wa pamba hai na mazingira ambapo unafanyika kwasababu wapo wadau wengi wanaotaka kununua pamba hai hasa ikizingatia kuwa Tanzania ndio nchi inayoshika namba moja Afrika kwa uzalishaji wa pamba hai na kuwepo na mahitaji makubwa.
"Kama mnavyokumbuka wiki moja au mbili zilizopita rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara katika Mkoa wa Singida alizungumzia suala la uboreshaji wa mazingira kwa hiyo mradi huu umekuja muda mwafaka," alisema.
Aliongeza kuwa mradi huu unafanyika katika mikoa hii kwasababu takwimu zinaonyesha kuwa mikoa ya Simiyu na Singida wakulima wanazingatia kilimo cha pamba hai.
Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Kijani Hai kutoka Shirika la GIZ, Hendrick Buermann, alisema wameamua kuja na mradi huu kwasababu kwa miaka sita mfululizo wakuluna katika mikoa ya Singida na Simiyu wanatekeleza kilimo hai kwa kushirikisha zaidi ya wakulima elfu sita.
Buermann alisema kupitia kilimo hai wakulima wameweza kunufaika kwa kuongeza uzalishaji na kupata soko la uhakika la mazao yao kwasababu hawatumii madawa katika uzalishaji.
0 Comments