![]() |
Mhe. Abdalah Ulega; Waziri wa Mifugo na Uvuvi |
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega amesema kuwa wizara yake itahakikisha inaweka mazingira bora ya kufuga, kusindika na kufanya biashara ya mazao yatokanayo na mifugo na uvuvi na makundi yote katika mnyororo mzima wa thamani.
Ulega aliyasema hayo wakati akifungua kongamano la 46 la chama cha wazalishaji na wataalamu wa mifugo na uvuvi Tanzania(TSAP) kinachoendelea mkoani Arusha ambapo alisema kuwa ni wakati muafaka wa kufanya mapinduzi katika mnyororo mzima wa thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora kwa wananchi na masoko yanayowazunguka.
Alisema kuwa wizara inatilia mkazo katika uwekezaji wa malisho na mbegu kwani kuna uhitaji mkubwa wa rasilimali hizo ikiwemo vyakula bora vya mifugo na samaki, vifaranga bora wa kuku, nyama bora ya ng'ombe, maziwa na bidhaa zake.
“Nawahimiza wafugaji na wazalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kuwekeza katika teknolojia za kisasa na vitendea kazi sahihi vitakavyoongeza uzalishaji wa mifugo na uvuvi,” Alisema Ulega.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wazalishaji na wataalamu wa mifugo na uvuvi Tanzania(TSAP) Dkt, Jonas Kizima alisema kuwa kwa sasa chama hicho kina wanachama 300 na lengo likiwa ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya mifugo na uvuvi lakini pia kushirikiana na wataalamu wa sekta zote.
Dkt. Kizima alieleza kuwa katika mkutano huo wa siku tatu wataweza kuwasilisha makala 36 za kisayansi ikiwa ni pamoja na mada 2 za kitaifa na kujadiliwa na wanachama wote.
Naye mtendaji mkuu wa chama hicho George Msalia alisema kuwa kama wataamu wanataka kutoa mchango kwa sekta hizo mbili ili ziendelee kutoa mchango katika uchimi wa nchi na kwa wananchi wetu.
“Ndio wataalamu tunaofanya kazi na wafugaji na wavuvi lakini pia na watu wanaofuga samaki, tunawapa ushauri mbalimbali na tunakutana mara moja kwa mwaka kuzungumza habari za kisekta, kuangalia tulikotoka na tunakokwenda, tuna changamoto gani na wapi tuendelee kujipanga,” Alieleza.
0 Comments