Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Jumla ya magari matano ya Mbao yamekamatwa na mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya kuuza risiti feki za kielektroniki na kuikosesha serikali mapato.
Meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe Specioza Owure,amesema wafanyabiashara hasa wa mbao mkoani hapa wanaongoza kwa kuuza risiti mitaani jambo ambalo halivumiliki.
Owure ametoa ripoti hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,kwenye uzinduzi wa kampeni ya TUWAJIBIKE yenye lengo la kuhamasisha walipa kodi na wateja kutoa na kudai risiti halisi za kielektroniki pindi wanapouza na Kununua bidhaa.
Meneja msaidizi upande ukaguzi Sylivester Nzali na meneja msaidizi upande wa huduma kwa mlipa kodi Beatrice kahoho wamesema kampeni hiyo ni endelevu kwa sababu wanataka kuhamasisha na kuelimisha matumizi sahihi ya mashine za EFD.
Kwa upande wa mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara halmashauri ya mji Njombe Eliud Pangamawe amesema kampeni hiyo ni nzuri kwa sababu wanahamasisha wafanyabiashara waweze kutoa risiti ili wachukue kodi ambayo ni kwa faida ya taifa zima huku akiwataka wafanyabiashara wenzake waache udanganyifu kwa wale wenye tabia hiyo.
Nao baadhi ya wafanyabiashara mjini Njombe akiwemo Evaristo Tave wamesema serikali kupitia mamlaka ya mapato TRA wameanzisha kampeni hiyo kwa ajili ya watu kulipa mapato halali na kwa uaminifu ili kujenga taifa na hivyo wako tayari kufuata maelekezo yote.
0 Comments