MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvester Koka amezitaka shule za msingi za msingi kuandaa wanafunzi ambao watashindana kwenye soko la kitaifa na kimataifa kwa kutumia teknolojia huku wakizingatia utamaduni wa Kitanzania.
Koka aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa mahafali ya shule za msingi za Kibaha Independence School (KIPS), Anex na Msangani zote zilizopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema kuwa shule zinapaswa kuwaandaa wanafunzi ili washindane kwenye soko la kitaifa na kimataifa na si wasome tu na kubaki na elimu ambayo haitaweza kuwadaidia katika maisha yao pia amewapongeza watu binafsi waliowekeza kwenye sekta ya elimu kwani ina mchango mkubwa sana na inaipunguzia serikali mzigo wa wanafunzi.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Njuweni Ltd Alhaj Yusuph Mfinanga ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa mwanafunzi atakayefaulu na kuongoza kitaifa kwenye mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka shule tatu zinazomilikiwa na kampuni hiyo.
Mfinanga amesema atawasomesha bure wanafunzi 20 watakaofaulu masomo ya kumaliza elimu ya msingi na kupata alama za daraja A kwa masomo yote ambapo watasoma kwenye shule za sekondari za kampuni hiyo za Vuchama Islamic Secondary School na Mangio Secondary School zilizopo Mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake meneja wa KIPS Nuru Mfinanga amesema kuwa wanashirikiana vizuri na serikali katika kukabiana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye sekta hiyo lengo likiwa ni kutoa elimu bora.
Mfinanga amesema kuwa wanaipunguzia mzigo serikali kwa kuwasomesha wanafunzi kupitia sekta binafsi na kuwataka wazazi kuwafuatilia watoto wao ili wafanye vizuri kwenye masomo yao na kuwataka walipe ada kwa wakati ili waweze kujiendesha na kutoa elimu bora. Jumla ya wanafunzi 109 walipewa vyeti vya kuhitimu elimu ya msingi.
0 Comments