YAELEZWA ITAENDA KUONGEZA UZALISHAJI WA ZAO HILO..
WAKULIMA WASEMA ITAENDA KUWAONGEZEA KIPATO..
Na Gift Mongi MATUKIODAIMA APP MOSHI.
Wakulima wa zao la ndizi katika jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro sasa wataweza kufanya kilimo biashara kupitia zao hilo kutokana na aina mpya ya miche inayosambazwa katika maeneo mbali mbali jimboni humo.
Miche hiyo aina ya Kimalindi ni ya kisasa na kuwa imekuwa ikizaa na kutoa mazao yenye tija ikilinganishwa na aina ya migomba kama hiyo iliyopo hivi sasa ambayo imeonekana kutokufanya vyema kwa wakulima.
Mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi amesema kuwa miche hiyo tayari ameigawa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali na kuwa imekuwa na uwezo wa kuvumilia magonjwa mbalimbali ya migomba tofauti na iliyopo hivi sasa.
'Leo naenda kukutana na madiwani wangu zaidi ya 20 na ninaenda kugawa aina hii mpya ya miche zaidi ya 100 ambayo wataenda kuiotesha katika maeneo yao na zoezi hili ni endelevu'amesema Prof Ndakidemi
Kwa mujibu wa mbunge huyo ni kuwa miche hiyo ikitunzwa vizuri huleta matokeo mazuri ambapo mkungu mmoja wa ndizi huweza kuwa na kilogramu kati ya 100 hadi 200.
Ameongeza kuwa miche hiyo kutokana na ukubwa wa shina lake pia ni chakula tosha kwa mifugo kwani kitakuwa chakutosha ikilinganishwa na migomba iliyopo hivi sasa.
'Wapo wadau wamejitolea kutusaidia aina hii ya migomba na hadi sasa tayari imefikia 3000 kati ya 5000 walioahidi kutusaidia katika eneo letu hili na lengo ni kumkwamua mkulima'anaeleza mbunge huyo ambaye pia ni mtaalam mbobezi katika kilimo.
Kadhalika Prof Ndakidemi amewataka wanufaika wa miche hiyo bora na ya kisasa kuweza kuigawa kwa wakulima wengine pindi itakapoanza kuchipua ili kuhakikisha wakulima walio wengi wanaweza kunufaika.
Inyasi Mushi ni diwani wa Kibosho kati ambapo anasema kupatikana kwa miche hiyo kutaenda kuleta suluhisho kwa wakulima jambo litakalopelekea waweze kulima kwa tija zaidi.
Naye Michael Makoy mkazi na mkulima wa Kibosho Sambarai amesema wakulima walio wengi wamekuwa wakishindwa kujikwamua kutokana na kukosa mbegu zinazozaa vizuri na kuwa ujio wa aina hiyo mpya ya miche ya migomba kutaenda kuleta mapinduzi kwa wakulima siku za usoni.
Mwisho.
0 Comments