Na abdallah Amir-Matukio Daima, Igunga.
WANANCHI wa Kata ya Iborogero Wilayani Igunga mkoani Tabora wamemtuhumu Diwani wao, Emmanuel Busongo wakidai amekuwa akiuza na kukodsha mashamba yao kwa wafanyabiashara kinyume cha utaratibu.
Hayo yamebainika juzi wakati wa ziara ya Mbunge wa Manonga, Seifu Khamis Gulamali (CCM) ambaye alikuwa jimboni humo kukagua shughuli za maendeleo sambamba na kutatua kero za wananchi ukiwemo mgogoro wa mashamba ya Kijiji cha Iborogero uliodumu zaidi ya miaka mitatu sasa.
Awali akizungumza kwa niaba ya wananchi kwenye mkutano huo wa hadhara, Jonas Machibya alimwambia Mbunge huyo kuwa diwani wao amekuwa akikodisha na kuuza mashamba ya Serikali ya kijiji na kusababisha kijiji hicho kukosa mapato ambayo yangesaidia kufanya shughuli za maendelo.
“Ndugu mbunge sisi wananchi wako tuna shida kwani huyu mheshimiwa diwani ameuza mashamba na mengine amekuwa akikodisha bila utaratibu” alisema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Baada ya shutuma hizo, Mbunge Gulamali alimwita kwenye jukwaa diwani kujibu tuhuma hizo ambapo diwani alikana kuwahi kuuza wala kukodisha mashamba hayo.
Katika hatua hiyo Gulamali alionya kwa kusema kuwa kila kiongozi anao wajibu wa kuheshimu mali za serikali pamoja na za wananchi waliomchaguwa hivyo yeye kama mbunge haamini kama diwani huyo amefanya hayo ambapo aliahidi kuyafuatilia na kurudisha majibu kwa wananchi.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwalamo Kata ya Iborogero, Mkulaba Makala alimwambia mbunge huyo kuwa wananchi wa kijiji hicho wameanza ujenzi wa shule ya msingi baada ya kuona watoto wao wanatembea umbali mrefu kufika shuleni.
Kufuatia ombi hilo la wananchi kujenga shule ya msingi katika kijiji chao, Mbunge huyo alikubali ambapo aliahidi kuchangia mifuko 200 ya simenti huku wakikubaliana kuwa shule hiyo itakapokamilika iitwe Shule ya Msingi Dk Samia Suluhu Hassani kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kuboresha elimu hapa nchini.
0 Comments