NA WILLIUM PAUL, ROMBO.
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga ametoa mitungi na majiko ya gesi kwa wakinamama wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro lengo likiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasani ya kuwatua mama kuni kichwani.
Akikabidhi mitungi hiyo kwa wajumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Rombo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ni wajibu wa kila mwananchi kutunza mazingira.
Alisema kuwa, Rais Dkt Samia Suluhu Hasani alianza na kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ambapo imefanikiwa katika maeneo mbalimbali nchini na sasa amekuja na kampuni ya kumtua mama kuni kichwani ili kutumia nishati rafiki katika kupikia.
"Nimekuja kumuunga mkono Rais wangu ambapo nimekuja na majiko na mitungi ya gesi nitakayowakabidhi ninyi Wajumbe ili muende kuwa mabalozi katika jamii na kuelimisha kuachana na Kuni na badala yake kutumia nishati rafiki kwa ajili ya kupikia" alisema Naibu Waziri Ummy.
Alisema kuwa, Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka UWT wilaya ya Rombo kumuunga mkono Rais Samia na kueleza kazi anazozifanya huku akiwataka kuhakikisha wanamtafutia kura ili aweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao wa 2025.
Aidha Naibu Waziri huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wilaya Rombo kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na kinamama.
"Natambua Rombo kunamatukio ya ukatili mengi hivyo nikuombe Mkuu wa wilaya kuwachukulia hatua wale wote wanaowafanya ukatili huo ili kuhakikisha vitendo hivi ambavyo vinachafua wilaya yetu vinakoma" alisema Naibu Waziri Ummy.
Pia alisema kuwa, wapo baadhi ya watu wenye ulemavu wakiwamo watoto wamekuwa wakifungia ndani na kuitaka jamii ya Rombo kuwaibua watu hao pamoja na kuendelea kuhamasisha jamii kuwapenda na kuwafariji kwani Serikali haipo tayari kuona kundi hilo likinyanyapaliwa.
Katika kuendelea kuunga mkono juhudi za kuongeza wanachama wapya katika Umoja huo Naibu Waziri huyo ametoa kadi 500 za Umoja huo kwa ajili ya wanachama wapya.
Mwisho...
0 Comments